Na, Ernest Magashi
Timu ya Mjimwema FC imefanikiwa kutwaa ubingwa wa mashindano ya KNK Cup 2026 ngazi ya Kata ya Namonge, Tarafa ya Siloka, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mhama FC katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Namonge.
Mchezo huo wa fainali uliokuwa na ushindani mkubwa uliwashuhudia Mjimwema FC wakionyesha kiwango kizuri na kuhakikisha wanamaliza safari yao ya mashindano hayo kwa kubeba taji la KNK Cup 2026 katika ngazi ya kata hiyo.
Diwani wa Kata ya Namonge, Mlalu Bundala, kwa niaba ya mdhamini wa mashindano hayo, Dkt. Doto Biteko, alikabidhi zawadi kwa washindi huku akiwapongeza wachezaji, viongozi wa timu na wananchi kwa kuunga mkono mashindano hayo.
Alieleza kuwa KNK Cup imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kukuza vipaji vya vijana, kuimarisha mshikamano wa wananchi pamoja na kuchochea maendeleo ya michezo katika Wilaya ya Bukombe.
Mabingwa wa Kata ya Namonge, Mjimwema FC, walikabidhiwa seti moja ya jezi, mpira mmoja pamoja na zawadi ya fedha taslimu shilingi 100,000, huku washindi wa pili, Mhama FC, wakipokea shilingi 50,000 pamoja na mpira mmoja.
Mashindano ya KNK Cup 2026 yanaendelea kuonyesha umuhimu wake katika kuibua vipaji vipya vya soka, kuwapa vijana fursa ya kuonyesha uwezo wao na kuimarisha maendeleo ya mchezo wa soka katika Wilaya ya Bukombe.

Comments
Post a Comment