Timu ya Machinga FC imeendelea kuonyesha ubora wake katika mashindano ya KNK Cup 2026 baada ya kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Mapinduzi FC katika mchezo wa tano wa michuano hiyo inauoendelea kutimua vumbi kwenye viwanja vya kata zote 17 za Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita.
Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa ulishuhudia timu zote mbili zikicheza soka la kuvutia, huku kila upande ukitafuta bao la kuongoza tangu dakika za mwanzo. Hata hivyo, ni Machinga FC waliopata furaha ya kwanza baada ya mshambuliaji wake, Chilunda Michael, kufunga bao pekee la mchezo katika dakika ya 32.
Baada ya bao hilo, Mapinduzi FC iliongeza kasi na kufanya mashambulizi ya mara kwa mara kutafuta bao la kusawazisha, lakini safu ya ulinzi ya Machinga FC ilisimama imara na kufanikiwa kuzuia hatari zote hadi mwamuzi alipomaliza mchezo.
Ushindi huo umeifanya Machinga FC kutanguliza mguu katika hatua inayofuata ya KNK Cup 2026, huku Mapinduzi FC ikiaga rasmi mashindano hayo baada ya kushindwa kugeuza matokeo.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Mwenyekiti wa Vijana wa UVCCM Kata ya Katente na mmoja wa wasimamizi wa mashindano hayo ngazi ya kata, Devid Jeremia, alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kuendelea kudhamini na kuandaa mashindano hayo ambayo yamekuwa chachu ya kuibua vipaji vya soka na kutoa burudani kwa wananchi.
Jeremia alisema KNK Cup imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuendeleza vipaji vya vijana, kuimarisha umoja na mshikamano wa jamii, pamoja na kuongeza ari ya michezo miongoni mwa wananchi wa Wilaya ya Bukombe.
Aidha, aliwahamasisha wananchi na mashabiki wa soka kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Michezo wa Katente kushuhudia michezo mingine ya KNK Cup 2026, huku akizitaka timu zinazoshiriki kuzingatia muda, sheria na kanuni za mashindano ili kudumisha nidhamu, ushindani wa haki na kuendeleza spirit ya michezo.

Comments
Post a Comment