Na, Ernest Magashi
Machinga FC imefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano ya KNK Cup 2026 baada ya kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Bomani FC katika mchezo wa hatua ya mtoano uliochezwa kwenye Uwanja wa Michezo wa Kata ya Katente, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita.
Bao pekee la mchezo lilifungwa na mshambuliaji Sweddy Kaguta katika dakika ya 36 ya kipindi cha kwanza, baada ya kutumia vyema nafasi aliyopata na kuiandikia Machinga FC bao lililodumu hadi mwisho wa mchezo.
Baada ya kufungwa, Bomani FC walirejea kipindi cha pili wakiwa na ari ya kusawazisha matokeo. Walitengeneza mashambulizi kadhaa na kulisakama lango la Machinga FC, lakini walishindwa kupenya ngome imara ya wapinzani wao iliyokuwa makini kuanzia safu ya ulinzi hadi kwa kipa.
Machinga FC nayo iliendelea kucheza kwa nidhamu na kutumia mashambulizi ya kushtukiza, huku ikilinda vyema bao lake hadi mwamuzi alipopuliza kipyenga cha mwisho, na kuthibitisha ushindi wa bao 1-0 uliowavusha moja kwa moja hatua ya robo fainali. Kwa matokeo hayo, Bomani FC imeaga rasmi mashindano ya KNK Cup 2026.
Mchezo huo ulihudhuriwa na mamia ya mashabiki waliojitokeza kushuhudia pambano lenye ushindani mkubwa na burudani ya hali ya juu. Baadhi yao walimpongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kuendelea kudhamini mashindano hayo ambayo yamekuwa yakikuza vipaji vya vijana, kuimarisha mshikamano wa jamii na kuchochea maendeleo ya michezo wilayani Bukombe.
Akizungumza baada ya mchezo, Afisa Mtendaji wa Kata ya Katente ambaye pia ni msimamizi mkuu wa mashindano katika kata hiyo, Elias Belege, aliwataka mashabiki kuendelea kushabikia kwa amani, upendo na ustaarabu, akisisitiza kuwa lengo la KNK Cup ni kuunganisha wananchi kupitia michezo na kutoa burudani salama kwa wote.
Belege pia alimshukuru Dkt. Doto Biteko kwa kuendelea kufadhili mashindano hayo, akieleza kuwa mbali na kuibua vipaji vya wachezaji, KNK Cup imekuwa chachu ya kukuza shughuli za kiuchumi kwa kuwavutia wafanyabiashara wadogo na kuwaunganisha wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Bukombe.

Comments
Post a Comment