LUFUNGA ACADEMY YAITOA KATENTE FC KWA MIKWAJU YA PENALTI 4-2 KWENYE LIGI YA KNK CUP 2026

Na,ErnestMagashi

ebukombesasablogspot.com.tz

Mashindano ya Ligi ya KNK Cup 2026 yameendelea leo katika siku yake ya pili kwa kutimua vumbi kwenye kata 17 za Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita. Katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Katente, timu ya Lufunga Academy iliibuka na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Katente FC kwa mikwaju ya penalti.Hatua ya mikwaju ya penalti ilifikiwa baada ya dakika 90 za mchezo kumalizika kwa sare ya bila kufungana (0-0). Kwa mujibu wa kanuni za mashindano ya KNK Cup 2026, kila mchezo lazima upatikane mshindi, hivyo timu hizo zililazimika kuamua matokeo kwa njia ya penalti.Katika mikwaju hiyo, kipa wa Lufunga Academy alifanya kazi kubwa kwa kudaka penalti mbili, huku timu yake ikifanikiwa kufunga penalti nne. Kwa upande wa Katente FC, walifanikiwa kufunga penalti mbili pekee, jambo lililoifanya Lufunga Academy kusonga mbele katika mashindano hayo na kuwaondoa Katente FC.Akizungumza baada ya mchezo huo, Mwenyekiti wa Vijana wa UVCCM Kata ya Katente, Devid Jeremia, ambaye ni mmoja wa wasimamizi wa mashindano hayo ngazi ya kata, alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kuendelea kuandaa mashindano hayo kila mwaka.Alisema mashindano hayo yamekuwa chanzo cha burudani kwa wananchi na fursa muhimu ya kuwaunganisha vijana kupitia michezo.

Aidha, Jeremia aliwahamasisha wananchi na vijana kuendelea kujitokeza kwa wingi kushuhudia michezo ya KNK Cup 2026 katika Uwanja wa Katente ili kupata burudani na kuendeleza ari ya kuunga mkono mashindano hayo.Pia, aliwataka wamiliki wa timu zinazoshiriki mashindano hayo kuhakikisha wachezaji wao wanafika viwanjani kwa wakati na kuzingatia sheria na taratibu zote za Ligi ya KNK Cup 2026.


Comments