Timu ya Kigos Rangers FC imeanza kwa kishindo mashindano ya Ligi ya KNK Cup 2026 baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Bodaboda FC katika mchezo wa kwanza uliochezwa katika Kata ya Katente, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita.
Nyota wa mchezo huo alikuwa mshambuliaji Aly Kasagula, ambaye alifunga mabao matatu (hat-trick) katika dakika za 7, 18 na 38 na kuiwezesha Kigos Rangers FC kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 3-0.
Katika kipindi cha pili, Kigos Rangers FC iliendelea kutawala mchezo ambapo Zachal Zachali aliongeza bao la nne dakika ya 52, kabla ya Jamali Jamali kufunga bao la tano dakika ya 88 na kukamilisha ushindi huo wa mabao 5-0.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Kata ya Katente, Devid Jeremia, aliwapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia mashindano ya KNK Cup, ambayo yamedhaminiwa na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko.
Jeremia alitoa wito kwa vijana na wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi katika michezo inayofuata, akieleza kuwa mashindano hayo ni sehemu ya burudani na kukuza vipaji vya vijana, na yataendelea hadi kupatikana bingwa wa Kata ya Katente atakayewakilisha kata hiyo katika ngazi ya tarafa.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Katente, Tabu Ng'hwani, aliwataka wachezaji na viongozi wa timu zote zinazoshiriki mashindano hayo kuzingatia kanuni na taratibu za ligi ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza, hususan suala la kuchelewa kufika uwanjani wakati wa michezo.

Comments
Post a Comment