Na, Ernest Magashi
Timu ya Kigos Rangers imeendelea kuonyesha kiwango bora katika mashindano ya KNK Cup 2026 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Lufunga Academy katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Michezo wa Kata ya Katente, Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita.
Ushindi huo umeiwezesha Kigos Rangers kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano hayo, huku Lufunga Academy ikiaga rasmi KNK Cup 2026.
Bao la kwanza la Kigos Rangers lilipatikana dakika ya 15 baada ya kipa wa Lufunga Academy, Daniel Mahugija, kujifunga. Bao hilo lilidumu hadi kipindi cha kwanza kumalizika.
Kipindi cha pili, Kaura Kaura aliisawazishia Lufunga Academy kwa kufunga bao dakika ya 56 na kuufanya mchezo kuwa mkali zaidi. Hata hivyo, mshambuliaji Majeshi Juma aliifungia Kigos Rangers bao la ushindi dakika ya 80 na kuipa tiketi ya kusonga mbele.
Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa ulihudhuriwa na mamia ya mashabiki waliojitokeza kushuhudia burudani ya soka. Mwamuzi Seleman Juma alisimamia mchezo kwa kuzingatia Sheria 17 za Mpira wa Miguu, huku akimwonyesha kadi nyekundu mchezaji mmoja wa Lufunga Academy dakika ya 82 baada ya kucheza faulo mbaya dhidi ya mpinzani wake.
Baadhi ya mashabiki waliohudhuria mchezo huo walimpongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kuendelea kudhamini mashindano ya KNK Cup, wakisema yamekuwa yakitoa burudani, kuibua vipaji vya vijana na kuimarisha mshikamano wa wananchi.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Mwenyekiti wa Vijana wa UVCCM Kata ya Katente na mmoja wa wasimamizi wa mashindano hayo ngazi ya kata, Devid Jeremia, alimpongeza Dkt. Biteko kwa kuendelea kuandaa mashindano hayo ambayo yamekuwa chachu ya kuendeleza vipaji vya soka na kutoa fursa kwa vijana kuonyesha uwezo wao.
Jeremia alisema KNK Cup imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kukuza vipaji vya vijana, kuimarisha umoja na mshikamano wa jamii.

Comments
Post a Comment