Mashindano ya Ligi ya KNK Cup 2026 yameendelea leo, Julai 3, 2026, katika siku yake ya tatu kwa kutimua vumbi kwenye kata 17 za Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita. Katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Katente, timu ya Katente United iliibuka na ushindi wa penalti 8-7 dhidi ya Bomani FC baada ya timu hizo kutoka sare ya mabao 1-1 katika dakika 90 za mchezo.
Katika mchezo huo, Bomani FC ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa mshambuliaji wake, Showa Sang'udi, aliyefunga dakika ya 10 na kuiweka timu yake mbele. Hata hivyo, Katente United ilirejea mchezoni kwa kusawazisha bao kupitia kwa Mariko Daud dakika ya 55, na kufanya mchezo huo kuwa na ushindani mkubwa hadi dakika ya mwisho.
Baada ya sare hiyo ya mabao 1-1 kudumu hadi kipenga cha mwisho cha mwamuzi, mshindi aliamuliwa kwa mikwaju ya penalti ambapo Katente United ilionyesha utulivu na umakini mkubwa na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa penalti 8-7, hivyo kutinga hatua inayofuata ya mashindano hayo.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Mwenyekiti wa Vijana wa UVCCM Kata ya Katente, Devid Jeremia, ambaye ni mmoja wa wasimamizi wa mashindano hayo ngazi ya kata, alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kuendelea kuandaa mashindano ya KNK Cup kila mwaka.
Alisema mashindano hayo yamekuwa chanzo kikubwa cha burudani kwa wananchi, yameimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa vijana, na kutoa fursa kwa vipaji vya michezo kuonekana na kuendelezwa.
Aidha, Jeremia aliwahamasisha wananchi na vijana kuendelea kujitokeza kwa wingi katika michezo ya KNK Cup 2026 inayofanyika kwenye Uwanja wa Katente ili kupata burudani na kuendeleza ari ya kuunga mkono mashindano hayo. Pia, aliwataka wamiliki wa timu zinazoshiriki kuhakikisha wachezaji wao wanafika viwanjani kwa wakati na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zote za ligi hiyo.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Katente, Paul Ng'hwani, alisema mashindano hayo yameleta chachu kubwa ya maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo, kwani yameongeza fursa za biashara kwa vijana na wananchi wanaouza vyakula, vinywaji na bidhaa mbalimbali kandokando ya uwanja wa michezo.
Mashindano ya KNK Cup 2026 yameendelea kuvutia mamia ya wananchi katika kata mbalimbali za Wilaya ya Bukombe, huku yakionekana kuwa jukwaa muhimu la kukuza vipaji vya michezo, kuimarisha mshikamano wa kijamii na kuchochea shughuli za kiuchumi katika jamii.

Comments
Post a Comment