KATENTE UNITED YAICHAPA KADI'S 2-1, YATINGA ROBO FAINALI YA KNK CUP 2026

Na, Ernest Magashi

ebukombesasablogspot.com.tz

Timu ya Katente United imeendelea kung'ara katika mashindano ya KNK Cup 2026 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kadi's FC katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Michezo wa Kata ya Katente, Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita.Ushindi huo umeiwezesha Katente United kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano hayo, huku Kadi's FC ikiaga rasmi KNK Cup 2026.Katente United ilianza kuonyesha makali yake mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya mshambuliaji wake kufunga bao la kuongoza dakika ya 35 na kuipeleka timu mapumzikoni ikiwa mbele kwa bao 1-0.Kipindi cha pili, mshambuliaji Deus Stela aliwaamsha tena mashabiki wa Katente United kwa kufunga bao la pili dakika ya 57 na kuipa timu yake uongozi wa mabao 2-0. Kadi's FC ilijitahidi kurejea mchezoni na kufanikiwa kupata bao la kufutia machozi kupitia kwa Neno Shure Boy dakika ya 87, lakini halikutosha kuiepusha timu hiyo na kipigo pamoja na kuaga mashindano.Mchezo huo ulihudhuriwa na mamia ya mashabiki walioshuhudia ushindani mkubwa na burudani ya soka, huku baadhi yao wakimpongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kuendelea kudhamini mashindano ya KNK Cup ambayo yamekuwa yakikuza vipaji vya vijana, kuimarisha mshikamano wa jamii na kuhamasisha maendeleo ya michezo wilayani humo.Akizungumza baada ya mchezo huo, Diwani wa Kata ya Katente na mmoja wa wasimamizi wa mashindano hayo ngazi ya kata, Kasuluzu Ng'hwani, alimpongeza Dkt. Biteko kwa kuendelea kuandaa mashindano hayo, akisema yamekuwa jukwaa muhimu la kuibua vipaji vya soka na kuwapa vijana nafasi ya kuonyesha uwezo wao.Ng'hwani alisema KNK Cup imeendelea kutimua vumbi kata zote 17 na kuwa chachu ya kukuza vipaji vya vijana, kuimarisha umoja na mshikamano wa wananchi wa Wilaya ya Bukombe, huku ikitoa burudani na kuongeza ari ya ushiriki katika michezo.

Comments