KATENTE UNITED NA KATENTE FC KUKUTANA FAINALI YA KNK CUP 2026, DABI YA KIHISTORIA KUTIKISA KATA YA KATENTE
Wananchi wa Kata ya Katente tarafa ya Ushirombo wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wanatarajia kushuhudia dabi ya kipekee na ya kusisimua pale Katente United itakapokutana na Katente FC kwenye mchezo wa fainali ya mashindano ya KNK Cup 2026, yatakayochezwa Julai 22, 2026, kwenye Uwanja wa Michezo Katente.
Katente FC ilikata tiketi ya kucheza fainali baada ya kuiondoa Machinga FC kwa mikwaju ya penalti 5-4 kufuatia timu hizo kutoka sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 za mchezo wa nusu fainali uliochezwa Julai 19, 2026.
Katika mchezo huo, timu zote zilionyesha ushindani mkubwa na kushambuliana kwa zamu, lakini zilishindwa kutikisa nyavu hadi dakika za kawaida kumalizika. Kwa mujibu wa Sheria za Mchezo, mwamuzi wa kati Selemani Juma aliamuru upigaji wa mikwaju ya penalti, ambapo Katente FC iliibuka na ushindi wa mabao 5-4 na kutinga hatua ya fainali.
Timu ya Katente United ilijihakikishia nafasi ya kucheza fainali hiyo baada ya kuichapa Kigos Rangers FC bao 1-0 katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa Julai 18, 2026 kwenye Uwanja wa Michezo Katente.
Bao pekee la ushindi lilifungwa na Avani Nzonzi katika dakika ya 38, bao lililoivusha Katente United hadi fainali huku likiiondosha Kigos Rangers FC kwenye mashindano ya mwaka huu.
Fainali hiyo inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwani timu zote mbili zinatoka mtaa mmoja wa namba moja kata ya Katente, jambo linaloifanya mechi hiyo kuwa dabi yenye historia na mvuto mkubwa kwa mashabiki wa soka.
Akizungumza kuelekea mchezo huo, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Kata ya Katente, David Jeremia, amewaalika wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia fainali hiyo, akisema itakuwa moja ya michezo yenye ushindani wa hali ya juu katika KNK Cup 2026.
Jeremia pia alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kuendelea kudhamini mashindano ya KNK Cup 2026, akieleza kuwa yamekuwa chachu ya kuibua vipaji vya vijana, kuimarisha mshikamano wa jamii na kutoa burudani kwa wananchi wa Bukombe na maeneo jirani.

Comments
Post a Comment