Timu ya Katente Star FC imeibuka mabingwa wa mashindano ya KNK Cup 2026 ngazi ya Kata ya Katente baada ya kuichapa Katente United FC kwa mikwaju ya penalti 4-3, kufuatia timu hizo kutoka sare ya bila kufungana (0-0) ndani ya dakika 90 za mchezo wa fainali.
Fainali hiyo ilikuwa ya ushindani wa hali ya juu, huku kila timu ikicheza kwa nidhamu, kujituma na kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga. Hata hivyo, washambuliaji wa pande zote walishindwa kuzitumia nafasi walizopata, na kuifanya mechi hiyo kumalizika kwa sare.
Kutokana na matokeo hayo, mwamuzi wa kati Seleman Juma aliamuru mshindi apatikane kwa mikwaju ya penalti. Katente Star ilionyesha utulivu na umakini mkubwa katika upigaji wa penalti na kufanikiwa kuibuka mabingwa kwa ushindi wa penalti 4-3.
Mchezo huo ulihudhuriwa na mamia ya mashabiki wa soka waliojitokeza kushuhudia fainali hiyo. Mkuu wa Kituo cha Polisi Ushirombo (OCS), Samson Kalilo, alimkabidhi nahodha wa Katente Star zawadi za ubingwa kwa niaba ya Diwani wa Kata ya Katente na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko.
Akizungumza baada ya kutwaa ubingwa, nahodha wa Katente Star, Magesa Malimi, alimshukuru Mungu pamoja na wachezaji wenzake kwa kujituma hadi kufikia mafanikio hayo. Alisema ushindi huo umetokana na mshikamano, nidhamu na kujituma kwa timu nzima, huku akieleza kuwa ni furaha kubwa kutwaa ubingwa wao wa kwanza tangu waanze kushiriki mashindano hayo mwaka 2016.
Kwa upande wake, nahodha wa Katente United, Zachal Daud, alisema walijiandaa vizuri na walikuwa na matumaini ya kutwaa ubingwa, lakini wamepokea matokeo hayo kwa moyo wa michezo kwani mpira wa miguu una matokeo ya aina yoyote.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Kata ya Katente, Devid Jeremia, alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kuendelea kudhamini mashindano ya KNK Cup, akisema yamekuwa jukwaa muhimu la kuibua vipaji vya vijana, kuimarisha mshikamano wa wananchi na kukuza maendeleo ya michezo katika Wilaya ya Bukombe.
Mabingwa Katente Star FC walikabidhiwa zawadi za ubingwa, seti moja ya jezi, mpira mmoja na kitita cha shilingi 100,000. Nao washindi wa pili, Katente United FC, walizawadiwa mpira mmoja pamoja na shilingi 50,000 kwa kutwaa nafasi ya pili.

Comments
Post a Comment