Timu ya Kadi's SC imeonyesha makali yake katika mashindano ya KNK Cup 2026 baada ya kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Kilimahewa FC katika mchezo wa nne wa michuano hiyo unaoendelea kupigwa katika viwanja vya kata zote 17 za Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita.
Mchezo huo ulikuwa wa ushindani mkubwa huku pande zote zikishambuliana kwa zamu kutafuta bao la mapema, lakini ni Kadi's SC waliotumia vizuri nafasi yao kupitia mshambuliaji Shabani Juma aliyetikisa nyavu katika dakika ya 53 na kuandika bao pekee la mchezo.
Licha ya Kilimahewa FC kuongeza kasi na kufanya mashambulizi ya kushtukiza katika dakika za mwisho, safu ya ulinzi ya Kadi's SC ilisimama imara na kufanikiwa kulinda bao hilo hadi mwamuzi alipopuliza kipenga cha mwisho.
Ushindi huo umeifanya Kadi's SC kutinga hatua inayofuata ya mashindano hayo, huku Kilimahewa FC ikiaga rasmi KNK Cup 2026.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Mwenyekiti wa Vijana wa UVCCM Kata ya Katente na mmoja wa wasimamizi wa mashindano hayo ngazi ya kata, Devid Jeremia, alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kuendelea kudhamini na kuandaa mashindano hayo ambayo yamekuwa yakileta burudani kubwa na kuibua vipaji vya soka kwa vijana wa Bukombe.
Jeremia alisema KNK Cup imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuibua wachezaji wenye vipaji, kuimarisha umoja na mshikamano wa wananchi, na kutoa burudani kwa wadau wa michezo wilayani humo.
Aidha, aliwahamasisha wananchi na mashabiki wa soka kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Michezo wa Katente kushuhudia michezo mingine ya KNK Cup 2026, huku akizitaka timu zinazoshiriki kuzingatia muda, sheria na kanuni za mashindano ili kudumisha nidhamu na ushindani wa haki badala ya malalamiko yasiyo ya msingi.

Comments
Post a Comment