Jayant Killa FC imeibuka bingwa wa mashindano ya KNK Cup 2026 ngazi ya Kata ya Runzewe Mashariki baada ya kuichapa Young Boy mabao 3-0 katika mchezo wa fainali uliochezwa Julai 18, 2026, kwenye Uwanja wa Michezo wa Runzewe Mashariki.
Ushindi huo umeihakikishia Jayant Killa FC tiketi ya kuiwakilisha kata hiyo katika hatua ya Tarafa ya Siloka.
Mshambuliaji Benedictho Julius aliifungia Jayant Killa FC bao la kwanza dakika ya 34 kabla ya winga mahiri Sizya Madikilo kuongeza la pili dakika ya 43 na kuwapa mashabiki furaha kubwa. Omary Assan alihitimisha karamu ya mabao kwa kufunga bao la tatu dakika ya 81 na kuthibitisha ubora wa mabingwa hao.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Runzewe Mashariki ambaye pia ni msimamizi mkuu wa mashindano hayo ngazi ya kata, Rashid Msalika, alisema jumla ya timu 13 zilishiriki mashindano yaliyoanza Julai 1, 2026 kwa mfumo wa mtoano.
Aliwapongeza mashabiki kwa kujitokeza kwa wingi na kushangilia kwa amani bila vurugu, huku akizisifu timu zote kwa kuonyesha nidhamu na ushindani wa hali ya juu hadi kufikia mchezo wa fainali.
Kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, Diwani wa Kata ya Runzewe Mashariki Mery Nchiba alikabidhi zawadi kwa washindi na kusema kuwa KNK Cup imeendelea kuwa chachu ya kuibua vipaji vya soka na kuwapa vijana nafasi ya kuonekana na timu za madaraja mbalimbali.
Alieleza kuwa Dkt. Biteko ameendelea kudhamini mashindano hayo kila mwaka tangu yalipokuwa yakijulikana kama Doto Cup 20216, yakilenga kukuza michezo, kuimarisha mshikamano wa wananchi na kuibua vipaji.
Nchiba aliwataka wachezaji wa Jayant Killa FC kuendelea kushirikiana ili kuiwakilisha vyema Kata ya Runzewe Mashariki katika hatua ya Tarafa ya Siloka, huku akizipongeza timu zote 13 zilizoshiriki kwa ushindani mzuri.
Nahodha wa Jayant Killa FC, Zabron Jonathan, alimshukuru Mungu pamoja na wachezaji wenzake kwa kujituma tangu mwanzo wa mashindano hadi kutwaa ubingwa, akisema sasa wanageukia maandalizi ya kusaka ubingwa wa Tarafa ya Siloka.
Kwa upande wake, nahodha wa Young Boy, Sinzya Mtunzya, alisema wanakubali matokeo ya mchezo huo na watajipanga upya kwa mashindano yajayo, huku akiahidi timu yao kumuunga mkono bingwa wa kata katika hatua inayofuata.
Katika zawadi zilizotolewa, Jayant Killa FC ilikabidhiwa seti moja ya jezi, mpira mmoja na shilingi 120,000, pamoja na motisha ya ziada ya shilingi 20,000 kutoka kwa Diwani Mery Nchiba. Young Boy, iliyomaliza nafasi ya pili, ilipokea mpira mmoja, shilingi 60,000 na motisha ya shilingi 10,000.

Comments
Post a Comment