Na, Ernest Magashi
Ilyamchele FC imefanikiwa kutwaa ubingwa wa mashindano ya KNK Cup 2026 ngazi ya Kata ya Ushirombo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Taiga FC katika mchezo wa fainali uliopigwa Julai 19, 2026 kwenye Uwanja wa Michezo Ushirombo.
Ushindi huo umeihakikishia Ilyamchele FC tiketi ya kuiwakilisha Kata ya Ushirombo katika hatua ya Tarafa ya Ushirombo, ikiwa na matumaini ya kuendeleza kiwango bora ilichoonyesha tangu kuanza kwa mashindano.
Mabao ya Ilyamchele FC yalifungwa na Kabwe Raymond dakika ya 14, Lazaro Kahesi dakika ya 37 na nahodha Visent Buyenze dakika ya 75. Kwa upande wa Taiga FC, mabao yalifungwa na Hussein Chuse dakika ya 70 na Antony Mwalyoyo dakika ya 72, lakini hayakutosha kuizuia Ilyamchele FC kutwaa taji hilo.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi, Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya KNK Cup 2026, Jonathan Mgaya, alimkaribisha Diwani wa Kata ya Ushirombo, Lameck Walangi, kukabidhi zawadi kwa washindi kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko.
Mgaya alimpongeza Dkt. Biteko kwa kuendelea kudhamini mashindano hayo na kuwapongeza timu zote zilizoshiriki, akiwataka kuendelea kushirikiana na kuongeza juhudi ili kufanya vizuri zaidi katika hatua zinazofuata za mashindano.
Kwa niaba ya Dkt. Biteko, Diwani wa Kata ya Ushirombo, Lameck Walangi, alisema KNK Cup imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuibua vipaji vya vijana na kuwapa nafasi ya kuonekana na timu mbalimbali za madaraja tofauti.
Aliongeza kuwa Dkt. Biteko ameendelea kudhamini mashindano hayo kila mwaka tangu yalipoanzishwa kwa jina la Doto Cup mwaka 2016, yakilenga kukuza michezo, kuimarisha mshikamano wa wananchi na kutoa fursa kwa vijana wenye vipaji.
Nahodha wa Ilyamchele FC, Visent Buyenze, alimshukuru Mungu pamoja na wachezaji wenzake kwa kujituma katika kila hatua ya mashindano hadi kufanikiwa kutwaa ubingwa. Alisema sasa nguvu zao zinaelekezwa katika maandalizi ya hatua inayofuata wakilenga kufanya vizuri na kusaka ubingwa wa tarafa.
Naye nahodha wa Taiga FC, Antony Mwalyoyo, alisema wanayaheshimu matokeo ya mchezo huo na watajipanga upya kwa mashindano yajayo. Pia aliiahidi Ilyamchele FC ushirikiano na sapoti katika hatua inayofuata ya mashindano.
Mbingwa Ilyamchele FC walikabiziwa seti moja ya jezi na mpira mmoja na fedha shilingi 100,000 hiku mshindi wa pili Taiga FC alipewa mpira mmoja na shilingi 50,000.

Comments
Post a Comment