Na, Ernest Magashi
Diwani wa Kata ya Uyovu, Tarafa ya Siloka, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Mathayo Kagoma, ameahidi kutoa shilingi milioni moja kwa mabingwa wa KNK Cup 2026 ngazi ya Kata ya Uyovu, Rane Academy, ikiwa ni motisha ya kujiandaa vyema na hatua inayofuata ya mashindano.
Ahadi hiyo ilitolewa Julai 16, 2026 wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, mdhamini wa mashindano hayo, baada ya mchezo wa fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Kata ya Uyovu.
Rane Academy ilitangazwa bingwa baada ya kuichapa Runzewe City kwa bao 1-0 katika mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa na uliovutia mamia ya mashabiki wa soka. Bao la ushindi lilifungwa na Thomas Emmanuel katika dakika ya 11 na kudumu hadi filimbi ya mwisho.
Akizungumza baada ya mchezo, mdau wa michezo wa Kata ya Uyovu, Peter Mganda, alimpongeza Diwani Kagoma kwa kuendelea kuunga mkono maendeleo ya michezo na kutoa motisha kwa timu itakayoiwakilisha kata katika hatua ya Tarafa.
Nahodha wa Rane Academy, Mbopa Nestory, alimshukuru Mungu pamoja na wachezaji wenzake kwa kujituma tangu kuanza kwa mashindano hadi kutwaa ubingwa. Pia alimshukuru Diwani Kagoma kwa ahadi ya shilingi milioni moja, akisema fedha hizo zitawasaidia kuweka kambi na kujiandaa kwa mashindano ya KNK Cup ngazi ya Tarafa.
"Tunamshukuru sana Diwani kwa kutuongezea nguvu. Ahadi hii itatupa morali ya kufanya maandalizi bora zaidi kwani lengo letu ni kutwaa ubingwa wa Tarafa na hatimaye kufika ngazi ya Jimbo," alisema Nestory.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Kata ya Uyovu ambaye pia ni msimamizi mkuu wa mashindano hayo, Petro Mkude, alimpongeza Dkt. Doto Biteko kwa kudhamini KNK Cup 2026 pamoja na Diwani Mathayo Kagoma kwa ushirikiano wake katika kufanikisha mashindano hayo.
Mkude alisema mashindano hayo yamefanyika kwa amani na mafanikio makubwa, huku timu zote zikionyesha nidhamu na ushindani wa hali ya juu ndani na nje ya uwanja.
Kwa ushindi huo, Rane Academy ilikabidhiwa seti moja ya jezi, mpira mmoja na zawadi ya shilingi 100,000, huku washindi wa pili, Runzewe City, wakipokea mpira mmoja na shilingi 50,000.

Comments
Post a Comment