Na, Ernest Magashi
Mkuu wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Mhadis Paskas Muragili, ametangaza rasmi bei za viingilio kwa wananchi na mashabiki wa soka watakaohudhuria Shamra Shamra ya Joto kuelekea msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2026/27, itakayofanyika Agosti 4, 2026 Bukombe Stadium.
Muragili alitangaza viingilio hivyo Julai 31, 2026, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika Bukombe Stadium, mtaa wa Kilimahewa, Kata ya Katente, mjini Ushirombo.
Alisema viingilio vitakuwa kama ifuatavyo: Mzunguko Shilingi 10,000Jukwaa la Ushirombo na Jukwaa la Siloka Shilingi 20,000VIP A Shilingi 50,000VIP B Shilingi 100,000VVIP Shilingi 150,000Aliongeza kuwa mashabiki watakuwa na uhuru wa kuchagua sehemu wanayotaka kukaa kulingana na tiketi watakazonunua. Tiketi zinapatikana kupitia mfumo wa mtandao pamoja na vituo mbalimbali vilivyoandaliwa.
Kwa mujibu wa Muragili, tiketi zinapatikana The One na Kitamba OG mjini Ushirombo. Nje ya Ushirombo, tiketi zinapatikana katika Mgodi wa Msasa, Katoro, Masumbwe na Geita Mjini.
Aidha, alisema kuna mpango wa kuongeza vituo vya mauzo katika maeneo ya Kahama, Chato na Mwanza kutokana na mahitaji ya mashabiki wengi wanaotarajiwa kuhudhuria tamasha hilo, kufuatia ushiriki wa klabu mbalimbali ikiwemo Yanga SC, ambayo inatarajiwa kutua kwa ndege Kahama kabla ya kuelekea Ushirombo.
Muragili aliwahimiza wananchi wa Bukombe na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki shamra shamra hizo, akisema burudani zitaanza saa 2:30 asubuhi na kuendelea hadi saa 3:00 usiku. Alibainisha kuwa mageti nane yatakuwa wazi ili kurahisisha mashabiki kuingia uwanjani kwa kutumia tiketi zao.
Aidha, alisema Bukombe Stadium imejengwa kwa viwango vya kisasa na ina uwezo wa kubeba mashabiki zaidi ya 5,000, wakiwemo zaidi ya 4,000 watakaokaa kwenye viti na zaidi ya 1,000 katika maeneo ya kusimama.
Naye Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Geita (GEREFA), Bosco Mwidad, alisema Bukombe Stadium ndiyo uwanja bora zaidi mkoani Geita na unatarajiwa kutumiwa na Geita Gold FC kama uwanja wake wa nyumbani katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2026/27.
Kwa upande wake, mkazi wa Ushirombo, Banunu Banunu, alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu mstaafu, Dkt. Doto Biteko, kwa kuendelea kuwaletea wananchi maendeleo makubwa, ikiwemo ujenzi wa uwanja huo wa kisasa ambao umefungua ukurasa mpya wa maendeleo ya michezo, kukuza vipaji vya vijana na kuchochea shughuli za kiuchumi katika Wilaya ya Bukombe.

Comments
Post a Comment