Ashanti FC imefanikiwa kutinga fainali ya KNK Cup 2026 ngazi ya Kata ya Bulangwa baada ya kuichapa Lufuna FC kwa mikwaju ya penalti 4-1 kufuatia sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 90 za mchezo wa nusu fainali uliochezwa katika Uwanja wa Michezo wa Kata ya Bulangwa.
Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa uliwashuhudia mamia ya mashabiki wakijitokeza kuzipa sapoti timu zao huku kila upande ukisaka tiketi ya kucheza fainali ya mashindano hayo.
Ashanti FC ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Pasinyo Joseph aliyetikisa nyavu dakika ya 37 na kuipeleka timu yake mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili, Lufuna FC ilirejea kwa kasi na kufanikiwa kusawazisha kupitia kwa Wilson Kapembe dakika ya 68. Jitihada za timu zote mbili kutafuta bao la ushindi hazikuzaa matunda hadi mwamuzi alipomaliza dakika 90 za mchezo zikiwa sare ya 1-1.
Kwa mujibu wa kanuni za mashindano, mshindi aliamuliwa kwa mikwaju ya penalti ambapo Ashanti FC ilionyesha utulivu na umakini mkubwa, ikishinda kwa penalti 4-1.
Kipa wa Ashanti FC, Daniel Mahugija, alikuwa shujaa wa mchezo baada ya kuokoa mikwaju miwili ya penalti ya Lufuna FC, huku wachezaji wenzake wakitumia vizuri nafasi zao na kuipa timu ushindi uliowapeleka moja kwa moja fainali ya KNK Cup 2026 ngazi ya kata.
Ushindi huo unaifanya Ashanti FC kuendelea kuonyesha ubora wake katika mashindano hayo, huku Lufuna FC ikihitimisha safari yake baada ya kupambana kwa kiwango kizuri lakini kushindwa kutumia vyema mikwaju ya penalti.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Kata ya Bulangwa na mmoja wa wasimamizi wa mashindano hayo ngazi ya kata, Peter Mkina, alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kuendelea kudhamini mashindano ya KNK Cup, ambayo amesema yamekuwa chachu ya kuibua vipaji vya vijana na kukuza soka wilayani Bukombe.
Mkina alisema mashindano hayo yameendelea kuimarisha umoja, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa wananchi, huku yakitoa fursa kwa wachezaji kujitangaza na kuvutia wadau mbalimbali wa michezo. Aidha, aliwataka wachezaji kuendelea kuzingatia nidhamu, kucheza kwa kufuata sheria za mchezo na kulinda heshima ya mashindano hayo hadi hatua ya fainali.

Comments
Post a Comment