Na, Ernest Magashi
Zaidi ya wagonjwa 700 wamenufaika na huduma za madaktari bingwa zilizotolewa katika Hospitali ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita ya kusogeza huduma za afya za kibingwa karibu na wananchi, hususan wa maeneo ya vijijini na pembezoni.
Akizungumza katika hafla ya kuwaaga madaktari bingwa hao, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Paskasi Muragili, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuboresha huduma za afya nchini na kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kibingwa bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.
Alisema hatua hiyo imepunguza gharama na muda wa wananchi kufuata matibabu ya kibingwa katika hospitali za rufaa na za mikoa.
“Serikali imewezesha upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa vinavyotumiwa na madaktari bingwa ili waweze kutoa huduma kwa ufanisi na weledi mkubwa,” alisema Mhandisi Muragili.
Aidha, aliipongeza timu ya madaktari bingwa kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kutoa huduma za afya za kibingwa na bobezi kwa wananchi wa Bukombe, pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa Hospitali ya Wilaya ya Bukombe kupitia mafunzo na ushirikiano wa karibu wakati wa utoaji wa huduma.
Mhandisi Muragili aliwataka wananchi waliopata huduma hizo kuwa mabalozi wazuri kwa kueleza mafanikio ya Serikali katika kuboresha sekta ya afya na kusogeza huduma muhimu karibu na wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Adelina Mfikwa, aliwapongeza wananchi wote waliojitokeza kupata huduma hizo, akisema hatua hiyo imewawezesha kupata matibabu ya kibingwa ndani ya wilaya yao na hivyo kuokoa muda na gharama ambazo zingetumika kufuata huduma hizo katika hospitali za mkoa au rufaa.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Bukombe, Dkt. Yohana Fumbuka, alisema huduma hizo za kibingwa zilianza kutolewa Juni 8, 2026 baada ya hospitali hiyo kupokea madaktari bingwa 22 kupitia mpango wa Madaktari Bingwa wa Rais Samia.
Alieleza kuwa madaktari hao walitoa huduma katika maeneo mbalimbali ya kibingwa na kuhitimisha zoezi hilo Juni 12, 2026, huku wagonjwa zaidi ya 700 wakihudumiwa.
Dkt. Fumbuka aliongeza kuwa wataalamu zaidi ya 87 wa afya kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe wamepata mafunzo na ujuzi wa ziada kupitia programu hiyo, hatua itakayosaidia kuimarisha utoaji wa huduma za kibingwa katika hospitali hiyo hata baada ya madaktari hao kuondoka.

Comments
Post a Comment