Timu za watani wa jadi, Yanga na Simba, leo zimefungua rasmi mashindano ya Ligi ya KNK Cup 2026 kwa mchezo wa kirafiki uliowakutanisha mashabiki wa timu hizo, ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 na kujinyakuria zawadi.
Mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa Shule ya Runzewe Sekondari kata ya Uyovu Wilaya ya Bukombe, ulivuta mamia ya mashabiki wa soka waliojitokeza kushuhudia pambano hilo la kusisimua, huku timu zote zikionyesha ushindani mkubwa kuanzia dakika za mwanzo hadi mwisho wa mchezo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo, Katibu wa KNK Cup, Domisian Kabalega, alisema ligi hiyo itaanza rasmi kutimua vumbi Julai 1, 2026, na itashirikisha jumla ya timu 242 kutoka kata 17 za Wilaya ya Bukombe.
Kabalega alisema lengo la mashindano hayo ni kuibua na kukuza vipaji vya vijana, kuimarisha mshikamano wa jamii na kuendeleza sekta ya michezo wilayani humo.
Pia aliwataka washiriki wote kuzingatia nidhamu katika kipindi chote cha mashindano ili kuenzi dhamira ya mwanzilishi wa mashindano hayo, Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko.
"Nidhamu, mshikamano na ushindani wa haki ndiyo nguzo kuu za mashindano haya. Tunawaomba washiriki wote kuyafanya mashindano haya kuwa ya mfano kwa kuzingatia maadili ya michezo," alisema Kabalega.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma, alisema KNK Cup imekuwa chachu ya maendeleo ya soka wilayani humo, akibainisha kuwa baadhi ya vijana waliopitia mashindano hayo tayari wanashiriki katika timu mbalimbali zinazoshiriki mashindano ya kitaifa.
Aidha, Kagoma aliwataka vijana kutumia mashindano hayo kama jukwaa la kuonesha vipaji vyao, kujipatia fursa za ajira kupitia michezo, kujenga afya bora na kuimarisha umoja na mshikamano katika jamii.
Mashindano ya KNK Cup 2026 yanatarajiwa kuwa miongoni mwa mashindano makubwa ya ngazi ya wilaya, yakikusanya mamia ya vijana kutoka maeneo mbalimbali ya Bukombe kwa lengo la kuendeleza vipaji na kuhamasisha maendeleo kupitia michezo.

Comments
Post a Comment