SERIKALI YAENDELEA KUSOGEZA HUDUMA ZA KIJAMII BUKOMBE


Na, Ernest Magashi

ebukombesasablogspot.com.tz

Serikali imeendelea kuboresha na kusogeza huduma muhimu za kijamii kwa wananchi wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, ikiwemo sekta za afya, elimu, maji, umeme, barabara na miradi mingine ya maendeleo.Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Paskas Mragili, wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Ally Hapi, wilayani humo wiki hii.Mhandisi Mragili alisema kuwa katika kipindi cha miaka michache iliyopita, serikali imefanya maboresho makubwa katika sekta ya afya ambapo idadi ya zahanati imeongezeka kutoka zahanati nane hadi kufikia zahanati 23, ikiwa ni ongezeko la zahanati 15. Aidha, vituo vya afya vimeongezeka kutoka vitatu hadi saba.

Alisema kuwa licha ya wilaya hiyo kuwa na hospitali moja ya wilaya, hospitali hiyo imeboreshwa kwa kujengwa majengo mapya ya kutolea huduma, ikiwemo jengo la wazazi na watoto pamoja na vifaa vya kisasa vya tiba. 

Maboresho hayo yamewezesha hospitali hiyo kupokea madaktari bingwa wanane waliotoa huduma kwa wananchi wiki iliyopita.

Akizungumzia sekta ya elimu, alisema kuwa idadi ya shule za msingi zimeongezeka kutoka 80 hadi 100, sawa na ongezeko la shule 20. Vilevile, shule za sekondari za serikali zimeongezeka kutoka 16 hadi 30, ikiwa ni ongezeko la shule 14.Katika sekta ya maji, Mhandisi Mragili alisema kuwa mwaka 2021 upatikanaji wa maji mjini ulikuwa asilimia 47, lakini hadi mwaka huu umefikia asilimia 68. Kwa upande wa vijijini, upatikanaji wa maji umeongezeka kutoka asilimia 28 hadi kufikia asilimia 98, hatua aliyoieleza kuwa ni mafanikio makubwa kwa wananchi wa Bukombe.Kwa upande wa nishati ya umeme, alisema kuwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Mbunge wa Bukombe, Dkt. Doto Biteko, vitongoji vingi vimefikiwa na huduma ya umeme. Alibainisha kuwa mkandarasi anaendelea na kazi ya kupeleka umeme katika vitongoji vilivyosalia na kwamba vitongoji viwili pekee ndivyo havijafikiwa kwa sasa.Alisema kuwa TANESCO imekamilisha ujenzi wa jengo la utawala lenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 200 na linatarajiwa kuanza kutumika mwezi Julai mwaka huu.

Akizungumzia miundombinu ya barabara, Mhandisi Mragili alisema kuwa mwaka 2020/2021 wilaya hiyo ilikuwa na kilomita 3.7 za barabara za lami, lakini hadi sasa zimeongezeka na kufikia zaidi ya kilomita 9.9.Aidha, mtandao wa barabara za changarawe umeongezeka kutoka kilomita 193.3 hadi zaidi ya kilomita 478.6.

Aliongeza kuwa mwaka huu Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe imepokea zaidi ya shilingi bilioni 16.6 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.Akizungumza katika ziara hiyo, Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Dkt. Doto Biteko, alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa anazofanya katika kuboresha maisha ya wananchi wa Bukombe na Watanzania kwa ujumla.Dkt. Biteko alisema kuwa mafanikio yote yaliyotajwa ni matokeo ya uongozi thabiti wa Rais Samia ambaye amekuwa akitekeleza miradi ya maendeleo kwa vitendo."Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kiongozi anayejielekeza zaidi katika utekelezaji wa maendeleo kuliko maneno. Amefanya kazi kubwa ya kuibadilisha nchi na kusogeza huduma muhimu karibu na wananchi," alisema Dkt. Biteko.Aliongeza kuwa pamoja na miradi iliyotajwa, serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa barabara ya lami ya Ushirombo Katoro, soko la kisasa pamoja na stendi ya mabasi, mjini Ushirombo ambayo yote yatachochea ukuaji wa uchumi wa wananchi wa Bukombe.Dkt. Biteko aliwataka wanachama wa CCM kuendelea kueleza mafanikio ya serikali kwa wananchi na kusisitiza umuhimu wa malezi bora ya watoto kuanzia ngazi ya familia.Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa (MNEC), Ally Hapi, alisema ameridhishwa na utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Wilaya ya Bukombe na kupongeza juhudi za Mbunge Dkt. Biteko katika kusimamia maendeleo na kushirikiana na chama.Hapi alisema tangu alipowasili Bukombe ameshuhudia mshikamano mkubwa miongoni mwa wanachama wa CCM, jambo ambalo amesema linachangiwa na uongozi mzuri unaoshirikiana kwa karibu na serikali katika kuwatumikia wananchi.Aliwataka wanachama kuendelea kudumisha umoja, mshikamano na ushirikiano ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana.

Comments