Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita (RPC), Safia Jongo, amewakumbusha wananchi wa mkoa huo kuwa dhamana katika vituo vya polisi ni bure na hakuna mwananchi anayepaswa kutoa fedha ili kupata huduma hiyo.
Akizungumza wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, wilayani Nyang’hwale wiki iliyopita, RPC Jongo alisema wananchi wana haki ya kutoa taarifa za uhalifu, kufuatilia kesi zao na kupata dhamana kwa mujibu wa sheria bila kutozwa gharama yoyote.Alisisitiza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kusimamia sheria, kanuni na taratibu za utoaji huduma kwa wananchi kwa uwazi na haki.
Aidha, Kamanda Jongo alisema mtuhumiwa hatakiwi kukaa mahabusu kwa zaidi ya saa 24 isipokuwa kwa makosa yasiyokuwa na dhamana, yakiwemo mauaji na unyang’anyi wa kutumia silaha, ambapo hatua za kisheria hufuatwa kulingana na masharti yaliyowekwa.
Kauli hiyo ilipokelewa kwa furaha na wananchi wa Nyang’hwale, ambao walimpongeza RPC Jongo kwa kutoa elimu hiyo muhimu kwa umma.
Baadhi yao walisema taarifa hiyo imewasaidia kuelewa haki zao na kuondoa dhana potofu zilizokuwepo kuhusu dhamana katika vituo vya polisi.Wananchi hao walieleza kuwa elimu hiyo itasaidia kuongeza ushirikiano kati ya jamii na Jeshi la Polisi katika kudumisha amani, usalama na utawala wa sheria.

Comments
Post a Comment