RC AHIMIZA WATUMISHI WA UMMA KUFANYA KAZI KWA BIDII NA UADILIFU

Na, Ernest Magashi

ebukombesasablogspot.com.tz

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, amewahimiza watumishi wa umma katika halmashauri zote za mkoa huo kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa bidii, uadilifu na weledi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati na Serikali inaendelea kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa.Shigela ametoa wito huo wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kusikiliza na kutatua kero za wananchi Wilaya ya Bukombe.Katika ziara hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe kwa hatua nzuri iliyofikia katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, akisisitiza umuhimu wa miradi hiyo kukamilika kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya ubora vilivyowekwa na Serikali ili iweze kuanza kutoa huduma bora na zenye tija kwa wananchi.Aidha, alipokagua ujenzi wa Jengo la Utawala la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bukombe pamoja na Jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Shigela aliwataka viongozi wa taasisi hizo kuhakikisha wanatenga fedha za kutosha kwa ajili ya ununuzi wa samani na vifaa muhimu vya ofisi.Alisema hatua hiyo itawawezesha watumishi kufanya kazi katika mazingira bora, yatakayoongeza ufanisi, tija na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Paskasi Muragili, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayolenga kuboresha huduma za kijamii, mazingira ya kazi kwa watumishi na ustawi wa wananchi.

Mhandisi Muragili alisema uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali umeendelea kuleta mageuzi makubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu na utawala, hatua inayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Wilaya ya Bukombe na Mkoa wa Geita kwa ujumla.

Comments