Matumaini ya kuwafikia watu watatu wanaodaiwa kufukiwa na kifusi cha mchanga katika mgodi wa Madukajohn & Partners uliopo Kijiji cha Kelezia, Kata ya Igulwa, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, yameongezeka huku juhudi za uokoaji zikiendelea usiku na mchana.
Akizungumza na waandishi wa habari Juni 1, 2026, Meneja wa mgodi huo, Peter Joseph, alisema kuwa operesheni ya uokoaji imeanza kuonyesha mafanikio na kutoa matumaini makubwa ya kuwafikia watu hao katika muda mfupi ujao.
Alieleza kuwa tukio hilo lilitokea Mei 28, 2026 majira ya saa 9:00 alasiri, ambapo watu hao walifukiwa na kifusi walipokuwa ndani ya duwara namba 20 “B” wakifanya kazi ya kufunga matimba kwa kufuata maelekezo ya wakaguzi wa mgodi.
Joseph alisema tangu kuanza kwa operesheni hiyo Mei 29, 2026, waokoaji wamekuwa wakifanya kazi kwa zamu za mchana na usiku ili kuhakikisha wanafikia eneo walilopo waathirika haraka iwezekanavyo.
“Kwa sasa matumaini ni makubwa sana ya kuwafikia ndugu zetu. Endapo tutaendelea na kasi hii ya kazi usiku wa leo, tunaamini kesho tunaweza kuwafikia. Tunaendelea kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, huku tukimuomba Mungu awaongoze na kuwalinda Watanzania wenzetu ili tuweze kuwaokoa wakiwa salama,” alisema Joseph.
Aliwataja watu wanaodaiwa kufukiwa kuwa ni Renad Charles (29) na Juma Hussein (27), wote wakazi wa Masumbwe, pamoja na Ave Mchele (37), mkazi wa Kalole wilayani Mbogwe. Wote ni mafundi wa kufunga matimba mgodini humo.
Baadhi ya ndugu wa waliofukiwa, akiwemo Merina Wilson na Ernest Manyama, wamewaomba Watanzania kuendelea kuwaombea wapendwa wao ili waokoaji watakapowafikia waweze kuwakuta wakiwa hai na salama.
Operesheni ya uokoaji inaendelea huku wananchi wa eneo hilo na familia za waathirika wakifuatilia kwa karibu maendeleo ya juhudi hizo, wakitarajia kupata habari njema katika saa zijazo.

Comments
Post a Comment