MADIWANI NA WATENDAJI WAPIGWA MSASA USIMAMIZI WA KNK CUP 2026 BUKOMBE


Na, Ernest Magashi

ebukombesasablogspot.com.tz

Madiwani wa kata 17, madiwani wa viti maalumu, watendaji wa kata pamoja na wawakilishi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) ngazi ya kata katika Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wamepatiwa mafunzo maalumu ya usimamizi wa mashindano ya mpira wa miguu ya KNK CUP 2026, yanayodhaminiwa na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Doto Biteko.Akitoa mafunzo hayo, Mratibu wa Kamati ya Mashindano ya KNK CUP 2026, Bosco Mwidadi, alisema mashindano hayo yamekuwa yakifadhiliwa na Dkt. Biteko kila mwaka tangu mwaka 2016, ambapo hapo awali yalijulikana kama Doto Cup. Alisema mwaka 2024 yamefanyiwa maboresho na kubadilishwa jina kuwa KNK CUP 2026, yakibeba kaulimbiu ya Mbunge huyo isemayo, "Kusema Na Kutenda."Mwidadi alisema mashindano hayo yatazinduliwa Juni 28, 2026 katika Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Kata ya Uyovu, huku mchezo wa fainali ukitarajiwa kuchezwa katika Uwanja wa Kisasa wa Kilimahewa uliopo mjini Ushirombo.Alieleza kuwa lengo la kuanzishwa kwa mashindano hayo ni kuwaunganisha wananchi kupitia michezo, kuchochea fursa za kiuchumi na soko, pamoja na kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana kuanzia ngazi ya kijiji, kata, tarafa hadi wilaya. Aliongeza kuwa bingwa wa mashindano hayo atapata nafasi ya kushiriki ligi ya daraja la nne ngazi ya wilaya.Kwa mujibu wa Mwidadi, jumla ya timu 242 zimesajiliwa kushiriki mashindano hayo na zitacheza kwa mfumo wa mtoano kuanzia ngazi ya vijiji, kata na tarafa nne za kisoka zilizopo wilayani humo. Alisema jumla ya michezo 320 inatarajiwa kuchezwa hadi kufikia fainali.

Aidha, alisema kamati ya mashindano imewashirikisha wataalamu wa michezo kutoka Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya, Afisa Michezo wa Wilaya na wadau wengine ili kuhakikisha mashindano hayo yanaendeshwa kwa weledi.

 Pia, watendaji wa kata watasimamia uratibu wa mashindano katika maeneo yao, huku vijana wa UVCCM wakitarajiwa kuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya mashindano hayo.Mwidadi alibainisha kuwa waamuzi tayari wamepewa mafunzo maalumu kuhusu sheria 17 za mpira wa miguu pamoja na kanuni za uendeshaji wa KNK CUP na wamekabidhiwa vifaa vya kazi, wakisubiri uzinduzi rasmi wa mashindano hayo.Akizungumza katika semina hiyo, Mtendaji wa Kata ya Runzewe Magharibi, Amos Obed, aliwataka watendaji wenzake ambao si wazoefu wa mashindano hayo kushirikiana na wenzao ili kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa na Mbunge yanafikiwa.Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Butinzya, Kwizi Mathias, alimpongeza Dkt. Biteko kwa maono yake makubwa ya maendeleo, hususan katika sekta ya michezo ambayo imekuwa chachu ya kuibua vipaji vya vijana wengi wa Bukombe.Naye Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Benjamin Mgeta, alisema lengo kuu la kuanzishwa kwa KNK CUP ni kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi wa Wilaya ya Bukombe.Mgeta aliwataka wasimamizi wa mashindano hayo kutoruhusu vitendo vya vurugu na migogoro, huku akiwahimiza madiwani kuwepo viwanjani mara kwa mara ili kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza na kuondoa malalamiko yasiyo ya lazima.Pia aliwataka viongozi wa UVCCM kuhakikisha wanakuwa chachu ya hamasa, amani na mshikamano katika mashindano hayo badala ya kuwa chanzo cha migogoro, ili KNK CUP 2026 iwe mfano wa mafanikio na maendeleo ya michezo katika Wilaya ya Bukombe zawadi zitatolewa kuazia mshidi wa kwanza na wapili kuazia kata na Tarafa na wilaya. 

Comments