Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wamempongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu mstafu, Dkt. Doto Biteko, kwa kuendelea kudhamini mashindano ya mpira wa miguu wilayani humo tangu alipochaguliwa kuwa mbunge mwaka 2015.
Pongezi hizo zilitolewa na madiwani mbalimbali wakati wa uzinduzi wa Ligi ya KNK Cup 2026 uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Runzewe, Kata ya Uyovu.
Diwani wa Kata ya Uyovu, Mathayo Kagoma, alisema Dkt. Biteko amekuwa chachu ya maendeleo makubwa ya michezo wilayani Bukombe kupitia mashindano hayo ambayo hapo awali yalijulikana kama Doto Cup kabla ya kubadilishwa jina na kuwa KNK Cup.
Alisema mashindano hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kuibua vipaji vya vijana, kutoa fursa za ajira kupitia michezo na kuimarisha afya za wananchi.
Kagoma aliongeza kuwa kufanyika kwa uzinduzi wa mashindano hayo katika Kata ya Uyovu ni heshima kubwa kwa wananchi wa eneo hilo, huku akieleza matumaini yake kuwa timu za kata hiyo zitafanya vizuri na kuwania ubingwa wa mwaka huu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo, Katibu wa KNK Cup, Domisian Kabalega, alisema ligi hiyo itaanza rasmi Julai 1, 2026, ikishirikisha jumla ya timu 248 kutoka kata 17 za Wilaya ya Bukombe.
Kabalega alisema lengo la mashindano hayo ni kuibua na kukuza vipaji vya vijana, kuimarisha mshikamano wa jamii na kuendeleza sekta ya michezo wilayani humo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma, alisema KNK Cup imekuwa chachu ya maendeleo ya soka wilayani Bukombe, akibainisha kuwa baadhi ya vijana waliopitia mashindano hayo tayari wanacheza katika timu mbalimbali zinazoshiriki ligi na mashindano ya kitaifa.
Aidha, aliwataka vijana kutumia mashindano hayo kama jukwaa la kuonesha vipaji vyao, kujipatia fursa za ajira kupitia michezo, kujenga afya bora na kuimarisha umoja na mshikamano katika jamii.
Mkazi wa Kata ya Uyovu, Piter Shaban, aliungana na madiwani hao kumpongeza Dkt. Biteko kwa mchango wake mkubwa katika sekta ya michezo.
Alisema kuwa tangu aingie bungeni mwaka 2015, wananchi wa Bukombe wamekuwa wakinufaika na burudani ya mpira wa miguu kupitia mashindano hayo, sambamba na utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo katika jimbo hilo.
Mashindano ya KNK Cup 2026 yalizinduliwa kwa mchezo wa kirafiki uliowakutanisha mashabiki wa timu za Yanga na Simba. Katika mchezo huo, timu ya Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba na kujinyakulia zawadi ya kwanza ya mashindano hayo.

Comments
Post a Comment