Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, amewataka watendaji wa Tume ya Madini nchini kuendelea kuimarisha usimamizi wa Sekta ya Madini kwa kusimamia ipasavyo leseni za uchimbaji, kutatua migogoro kwa wakati na kuongeza ushiriki wa Watanzania katika shughuli za mnyororo wa thamani wa madini ili sekta hiyo iendelee kutoa mchango mkubwa katika uchumi wa taifa.
Mhandisi Samamba alitoa maelekezo hayo wakati akifungua kikao cha Menejimenti ya Tume ya Madini kilichofanyika mkoani Morogoro, ambapo alisisitiza umuhimu wa Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuhakikisha leseni zinazotolewa kwa wachimbaji zinaendelezwa kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa.Alibainisha kuwa Serikali haitasita kufuta leseni ambazo hazijaendelezwa na kuzipatia wawekezaji au waombaji wenye uwezo na dhamira ya kuziendeleza kwa manufaa ya taifa.
Aidha, aliwataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kushughulikia migogoro inayojitokeza katika maeneo ya uchimbaji kwa wakati, kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo, badala ya kusubiri migogoro hiyo kufikishwa katika ngazi za juu za maamuzi.
Katika kikao hicho kilichoshirikisha viongozi wa taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara ya Madini, akiwemo Kamishna wa Madini, Dkt. Abdulrahman Mwanga, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, pamoja na wakurugenzi, mameneja na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, Mhandisi Samamba aliipongeza Tume ya Madini kwa kuvuka malengo ya ukusanyaji wa maduhuli.
Alisema kuwa kuanzia Julai 2025 hadi sasa, Tume ya Madini imekusanya shilingi trilioni 1.36, sawa na asilimia 113.34 ya lengo la mwaka wa fedha 2025/2026. Aliwataka watendaji kuendelea kubuni mikakati mipya itakayowezesha Tume kuvuka lengo la kukusanya shilingi trilioni 1.4 katika mwaka wa fedha 2026/2027
Katibu Mkuu huyo pia alielekeza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuweka mkazo katika usimamizi wa afya, usalama na utunzaji wa mazingira kwenye maeneo ya uchimbaji wa madini. Alisisitiza umuhimu wa kutoa elimu endelevu kwa wachimbaji wadogo na kuimarisha ukaguzi wa shughuli za uchimbaji ili kupunguza ajali na madhara ya kimazingira.
Akizungumzia jitihada za Serikali za kudhibiti utoroshaji wa madini, Mhandisi Samamba alisema mikakati iliyowekwa ni pamoja na kuimarisha usimamizi katika mnyororo mzima wa thamani wa madini kuanzia uzalishaji hadi usafirishaji, kuendelea kuanzisha masoko na vituo vya ununuzi wa madini, kuweka bei elekezi zinazozingatia hali ya soko la dunia, pamoja na kuondoa baadhi ya vikwazo vya tozo na kodi vinavyoathiri biashara ya madini.
“Kwa kushirikiana na Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, Tume ya Madini imeendelea kutoa elimu ya uzalendo kwa wadau wa sekta hii ili wawe mabalozi wazuri wa rasilimali za taifa. Hii ni muhimu hasa ikizingatiwa kuwa wachimbaji wadogo wanachangia takribani asilimia 40 ya mapato ya sekta ya madini,” alisema Mhandisi Samamba.
Aidha, alisema Serikali imeidhinisha kutengwa kwa asilimia 10 ya mapato yanayotokana na Sekta ya Madini kwa ajili ya kugharamia tafiti za kina za madini, hatua inayotarajiwa kuongeza ugunduzi wa rasilimali mpya na kuchochea uwekezaji zaidi katika sekta hiyo.
Akihitimisha hotuba yake, Mhandisi Samamba aliwataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuendelea kuisimamia sekta hiyo kwa uzalendo, uwajibikaji na ubunifu ili kuhakikisha wananchi wananufaika ipasavyo na rasilimali za madini.
Kwa upande wake, Kamishna wa Madini, Dkt. Abdulrahman Mwanga, alimpongeza Mhandisi Samamba kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano na mshikamano kati ya taasisi zilizo chini ya Wizara ya Madini, jambo ambalo limechangia kuimarika kwa utendaji na maendeleo ya sekta hiyo nchini.
Naye Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo, aliishukuru Wizara ya Madini kwa kuendelea kuboresha mazingira ya kazi kupitia upatikanaji wa vifaa mbalimbali, ikiwemo magari na mashine za kisasa za kupima madini ya metali.
Alisema Tume ya Madini itaendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali kwa ufanisi ili kufikia matarajio ya wananchi na kuchangia maendeleo ya taifa kupitia Sekta ya Madini.

Comments
Post a Comment