DKT. BITEKO APONGEZWA KWA ZIARA YA KUWASHUKURU WANACHAMA WA CCM KATA 17 BUKOMBE


Na, Ernest Magashi

ebukombesasablogspot.com.tz

Mbunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Doto Biteko, amepongezwa kwa kutenga muda wake kufanya ziara katika kata 17 za Jimbo la Bukombe kwa lengo la kuwashukuru wanachama wa CCM baada ya uchaguzi mkuu.Pongezi hizo zimetolewa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Ally Hapi, wakati akitoa semina elekezi ya wanachama wa CCM kupitia Jumuiya ya Wazazi iliyofanyika katika ukumbi wa CCM Wilaya ya Bukombe.Akizungumza katika semina hiyo, Hapi alisema wanachama wa CCM Bukombe wameonyesha mshikamano mkubwa na ushirikiano kwa mbunge wao, huku akibainisha kuwa Dkt. Biteko ni miongoni mwa wabunge wachache waliofanya ziara ya kuwashukuru wanachama mara baada ya uchaguzi mkuu."Wanachama mmenifurahisha sana kwa mshikamano wenu. Ukweli ni kwamba mbunge mliyenaye ni miongoni mwa viongozi wachache waliofanya ziara ya kuwashukuru wanachama baada ya uchaguzi mkuu. Hakika Dkt. Biteko anatekeleza vizuri Katiba na kanuni za chama," alisema Hapi.

Aidha, aliwataka wanachama kuendelea kuimarisha mshikamano ndani ya chama kwa kushuka hadi ngazi za chini za jumuiya na kutoa elimu itakayosaidia kuimarisha chama pamoja na kuwafikia wanachama wote.Hapi pia alisisitiza umuhimu wa viongozi wa Jumuiya ya Wazazi kushirikiana katika kuendeleza malezi bora kwa watoto kwa kuzingatia kaulimbiu ya jumuiya hiyo inayosema, "Malezi Bora na Uzalendo ni Msingi wa Taifa." Alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kujenga taifa lenye vijana wenye maadili mema na kupunguza mmomonyoko wa maadili katika jamii.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukombe, Luhanda Lutonja, alisema chama hicho kinaendelea kuwa imara wilayani humo kutokana na ziara mbalimbali za uhai wa chama zinazofanyika mara kwa mara pamoja na ushirikiano mzuri uliopo kati ya chama na jumuiya zake.Lutonja alimpongeza Dkt. Biteko kwa kazi kubwa anayofanya ya kusukuma maendeleo ya wananchi wa Bukombe, akieleza kuwa ziara yake ya kuwashukuru wanachama ilianza Aprili 7, 2026 na kuhitimishwa Mei 23, 2026. 

Kupitia ziara hiyo, Dkt. Biteko aliwashukuru wanachama wa CCM kwa kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, yeye mwenyewe pamoja na madiwani wa chama hicho.Akizungumza katika semina hiyo, Dkt. Biteko alisema Bukombe inaendelea kupiga hatua za maendeleo kutokana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.Aliwaomba wanachama wa CCM kuendelea kuyaishi maelekezo yaliyotolewa na viongozi wa chama na jumuiya zake ili kuimarisha mshikamano, umoja na malezi bora kwa watoto.Akizungumzia maendeleo ya jimbo hilo, Dkt. Biteko alimpongeza Rais Dkt. Samia kwa kuendelea kupeleka fedha za maendeleo Bukombe, ambazo zimewezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali katika sekta za afya, elimu, barabara, umeme na maendeleo mengine ya kijami.

Comments