DKT. BITEKO AHIMIZA WAZAZI KUIMARISHA MALEZI BORA KWA WATOTO


Na, Ernest Magashi

ebukombesasablogspot.com.tz

Mbunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Dkt. Doto Biteko, amewataka wazazi na walezi kuendelea kuimarisha malezi bora kwa watoto ili wakue katika maadili mema yanayozingatia mila na tamaduni za Kitanzania.Wito huo ameutoa leo alipokuwa akizungumza katika semina ya Jumuia ya Wazazi ya CCM iliyofanyika Wilaya ya Bukombe, wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Jumuia hiyo Taifa na MNEC, Ally Hapi.Dkt. Biteko alisema kuwa malezi bora ni msingi wa kujenga taifa lenye wananchi wenye maadili na uzalendo, hivyo ni wajibu wa wazazi na wanachama wa CCM kuwajenga watoto katika misingi ya nidhamu, uchapakazi na uwajibikaji kwa manufaa ya familia na taifa kwa ujumla.Aidha, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kupeleka fedha nyingi za utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Bukombe.“Tunampenda Rais Dkt. Samia kwa sababu amekuwa akifanya kazi kubwa ya kuwaletea wananchi maendeleo. Tofauti yake na wengine ni kwamba huzungumza kidogo lakini hutenda zaidi. Ameendelea kuboresha huduma za kijamii na kutoa fursa kwa wachimbaji wa madini,” alisema Dkt. Biteko.

Alisema serikali imeleta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya lami kutoka Ushirombo hadi Katoro, pamoja na barabara za mjini Ushirombo na Kata ya Uyovu, sambamba na kuboresha sekta za afya na elimu.Dkt. Biteko aliwataka wanachama wa CCM kuendelea kufanya kazi na kutembelea matawi ya chama badala ya kusubiri ugeni.

“Sisi tuwe mfano wa uchapakazi ili wananchi waendelee kukiamini chama na serikali. Bukombe inaendelea kusonga mbele kimaendeleo kupitia ushirikiano na Serikali ya Awamu ya Sita,” alisema.Akizungumza kuhusu utekelezaji wa Ilani ya CCM, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Paskas Mragili, alisema maendeleo yanayoonekana wilayani humo yanatokana na ushirikiano mzuri kati ya serikali, Mbunge Dkt. Biteko na madiwani.Alisema katika kipindi kifupi, idadi ya shule za msingi imeongezeka kutoka 80 hadi 100, huku shule za sekondari zikiongezeka kutoka 24 hadi 30. Aidha, Hospitali ya Wilaya imeendelea kuboreshwa na hivi karibuni madaktari bingwa wanane walitoa huduma za kibingwa kwa wananchi.

Mhandisi Mragili aliongeza kuwa zahanati na vituo vya afya vinaendelea kuongezeka, upatikanaji wa maji safi na salama umeimarika vijijini na mijini, huku barabara za changarawe na lami zikiendelea kujengwa.Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe hivi karibuni imepokea zaidi ya shilingi bilioni 16.6 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, nje na ujenzi wa soko la kisasa na stendi.Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Jumuia ya Wazazi ya CCM Taifa, Ally Hapi, alimpongeza Dkt. Biteko kwa utendaji wake mzuri wa kazi za ubunge na kwa kutafa katiba nankanuni za chama.Hapi alisema kutokana na utendaji huo, amependekeza Dkt. Biteko kuwa Mwenyekiti wa Wabunge wanaotokana na jumuia ya wazazi kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wazazi Taifa yatakayofanyika jijini Mwanza mwezi Julai 2026.

Alisema falsafa ya “Kusema na Kutenda” imejidhihirisha kupitia utendaji wa Dkt. Biteko, akimtaja kuwa ni kiongozi wa watu na mwenye kujali maendeleo ya wananchi.Kiongozi huyo wa kitaifa pia aliwapongeza wanachama wa CCM Bukombe kwa mshikamano wao na ushirikiano mzuri na serikali katika utekelezaji wa Ilani ya CCM.“Bukombe mmenifurahisha sana kwa umoja na mshikamano wenu. Nimeona miradi mingi mizuri inayotekelezwa, ikiwemo ujenzi wa soko na stendi za kisasa ambazo zitakuwa alama ya maendeleo kwa vizazi vijavyo,” alisema Hapi.

Aidha, aliwakumbusha wanachama kufuata katiba ya chama kwa kuwa waaminifu, kufanya kazi kwa bidii na kujiepusha na tabia zisizofaa kama uzururaji na ulevi.Akizungumzia malezi, Hapi alisema Jumuia ya Wazazi ina jukumu kubwa la kusimamia malezi kwa kuzingatia kaulimbiu ya jumuia hiyo isemayo: “Malezi Bora na Uzalendo ni Msingi wa Taifa.”Aliwataka viongozi wa jumuia kushuka ngazi za chini kuimarisha chama, kueleza mafanikio ya serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa malezi bora ili kukabiliana na mmomonyoko wa maadili kwa watoto.Naye Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi CCM Wilaya ya Bukombe, Hassan Mohamed, alisema jumuia hiyo imeendelea kufanya ziara katika ngazi za chini na kwamba wananchi wanajivunia maendeleo yanayopatikana chini ya uongozi wa Mbunge Dkt. Biteko.

Comments