Diwani wa Kata ya Katome, wilayani Bukombe mkoani Geita, Joseph Maganga, amechangia mabati 10 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa tawi la Kanisa la Ufunuo lililopo katika kata hiyo.
Maganga alisema mchango huo ni sehemu ya kuwasaidia waumini wa kanisa hilo katika juhudi zao za kukamilisha ujenzi wa nyumba ya ibada.
Akizungumza wakati wa ibada maalumu ya kuiombea Serikali iliyoongozwa na Askofu wa Makanisa ya Ufunuo Jimbo la Geita, Rosemeri Mashauri, Jumapili iliyopita, diwani huyo aliwahimiza waumini kuendelea kuiombea Serikali pamoja na viongozi wake ili waendelee kuwaletea wananchi maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Alisema ni muhimu kwa wananchi kuendelea kumwabudu Mungu na kuishi mafundisho yanayotolewa na watumishi wa Mungu ili kujenga jamii yenye maadili mema.
Ibada hiyo pia ilihudhuriwa na Mwenyekiti wa CCM Kata ya Katome, Erasto Masagwa, ambaye alimpongeza Askofu Mashauri kwa moyo wake wa upendo wa kutembelea makanisa na kuongoza maombi pamoja na kuhamasisha waumini kushirikiana na Serikali katika shughuli za maendeleo.
Kwa upande wake, Askofu wa Jimbo la Geita, Rosemeri Mashauri, alimshukuru Diwani Maganga kwa mchango wake wa mabati, akisema ni hatua inayodhihirisha ushirikiano mzuri kati ya viongozi na waumini wa kanisa.
Askofu Mashauri alisema ofisi yake nayo itaongeza mabati 10 ili kuharakisha kukamilika kwa ujenzi huo. Aidha, aliwahamasisha waumini kujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali badala ya kutegemea miujiza pekee bila kufanya kazi.
"Ndugu zangu wapendwa, wachungaji waelimisheni waumini kuwa mafanikio yanahitaji bidii na kazi halali. Mungu huwabariki watu kupitia biashara zao na kazi zao za kila siku," alisema Askofu Mashauri.
Katika hatua nyingine, aliwahimiza wazazi na walezi kuhakikisha watoto wote, wakiwemo wenye ulemavu, wanapata haki yao ya elimu badala ya kufichwa majumbani. Alisema elimu ni msingi muhimu wa maendeleo na kwamba vijana wanaohitimu masomo yao wanapaswa kujiandaa pia kujiajiri badala ya kutegemea ajira za Serikali pekee.
Askofu Mashauri aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali, madiwani, Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu mstafu Dkt. Doto Biteko, pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi.

Comments
Post a Comment