Timu ya Butinzya FC imeandika historia kwa kutwaa ubingwa wa mashindano ya Diwani Cup kwa mara ya kwanza baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Kazikazini FC katika mchezo wa fainali uliochezwa katika uwanja wa shule ya msingi Butinzya Juni 22, 2026.
Mashindano hayo yaliandaliwa na Diwani wa Kata ya Butinzya, Kwizi Chenya, kwa lengo la kuimarisha umoja, mshikamano na ushiriki wa vijana pamoja na wananchi katika shughuli za michezo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi kwa washindi wa kwanza hadi wa tatu, pamoja na washindi wa michezo mbalimbali ikiwemo mbio za mita 100 na mashindano ya kukimbiza kuku kwa wanaume na wanawake, Diwani Chenya aliwapongeza timu zote 10 zilizoshiriki mashindano hayo.
Alisema kuwa huu ni mwaka wa kwanza wa mashindano hayo na kwamba yataendelea kufanyika kila mwaka huku yakiboreshwa zaidi ili kuwapa wananchi burudani na fursa za kuonesha vipaji vyao.
"Mashindano haya ni mwanzo mzuri kwangu. Nimejifunza mengi tangu tulipozindua mwezi Mei hadi kufikia hitimisho lake leo Juni 22, 2026. Nawapongeza timu zote zilizoshiriki na mwaka ujao tutafanya maboresho makubwa zaidi," alisema Chenya.
Aliongeza kuwa Diwani Cup imehitimishwa ili kupisha maandalizi ya mashindano ya KNK Cup (Kusema Na Kutenda) yanayoandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, yanayotarajiwa kuanza Julai 1, 2026.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma, alimpongeza Diwani Chenya kwa ubunifu wake wa kuandaa mashindano hayo yaliyowakutanisha wananchi na vijana huku yakichochea maendeleo ya jamii.
"Huyu ni diwani mbunifu na mfano wa kuigwa. Ameonesha njia kwa madiwani wengine kwa kuanzisha mashindano haya muhimu. Hata mimi nimejifunza jambo kutoka kwake," alisema Kagoma.
Aidha, aliwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia mashindano ya KNK Cup yatakayoshirikisha kata zote 17 za Jimbo la Bukombe.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Runzewe Magharibi, Patrick Songolo, alisema amevutiwa na namna mashindano hayo yalivyoandaliwa na kuwashirikisha hata wazee kupitia michezo mbalimbali ikiwemo kukimbiza kuku na mbio za mita 100.
Nahodha wa Butinzya FC, Faida Lozalia, aliwashukuru wachezaji wenzake kwa kujituma na kupambana hadi kufanikisha ushindi huo.
"Ushindi huu umetokana na ushirikiano wetu pamoja na msaada wa Mungu. Tunamshukuru Diwani kwa kuandaa mashindano haya yaliyotupa hamasa kubwa ya kufanya vizuri," alisema Lozalia.
Naye Nahodha wa Kazikazini FC, Abery Hames, alisema licha ya kutopata ubingwa, timu yake imejifunza mengi na ina matumaini ya kufanya vizuri zaidi katika mashindano yajayo.
Mshindi wa tatu, timu ya Sinamila FC, kupitia nahodha wake Emmanuel Musa, alisema wamefurahishwa na nafasi waliyoipata na wanaamini siku zijazo wanaweza kufika fainali au kutwaa ubingwa.
Katika michezo mingine, Jackiline Christopher aliibuka mshindi wa mashindano ya kukimbiza kuku kwa wanawake na kujinyakulia zawadi ya kuku, huku Meshaki Lyangingwa akiibuka mshindi kwa upande wa wanaume.
Washindi hao walimpongeza Diwani Chenya kwa kuwajumuisha wazee katika michezo, jambo lililowapa fursa ya kushiriki shughuli za kijamii na kuimarisha afya zao.
Katika mbio za mita 100 kwa wanaume, Meshaki Lyangingwa aliibuka mshindi huku kwa wanawake ushindi ukienda kwa Jackiline Petro na kila mmoja alipata zawadi ya shilingi 20,000.
Kwa upande wa zawadi za mpira wa miguu, Butinzya FC ilikabidhiwa kombe, seti moja ya jezi, mpira mmoja na fedha taslimu shilingi 150,000. Mshindi wa pili, Kazikazini FC, alipatiwa shilingi 100,000 pamoja na mpira mmoja, huku Sinamila FC iliyomaliza katika nafasi ya tatu ikikabidhiwa shilingi 50,000 na mpira mmoja.

Comments
Post a Comment