Mradi wa ujenzi wa zahanati katika Kijiji cha Imalanguzu, Kata ya Bukombe mkoani Geita, ulioanzishwa kwa nguvu za wananchi kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, umepokea shilingi milioni 60 kutoka Serikalini kwa ajili ya kuukamilisha, ili wananchi waanze kupata huduma za afya karibu yao.
Hayo yameelezwa na Diwani wa Kata ya Bukombe, Rozaria Masokola, wakati wa ziara ya Mbunge huyo ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM. Ziara hiyo ililenga kuwashukuru wanachama wa CCM kwa kumchagua Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Mbunge na madiwani.
Masokola alibainisha kuwa ujenzi wa zahanati hiyo ulianza kwa nguvu za wananchi na kuungwa mkono na Dkt. Biteko, ambapo sasa unakamilishwa baada ya Serikali kutoa fedha hizo.
Alisema kukamilika kwa zahanati hiyo kutapunguza changamoto ya wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.
Aidha, alieleza kuwa Dkt. Biteko aliunga mkono jitihada za wananchi kwa kuchangia mifuko 200 ya saruji, mabati 250 na mbao 600, ambapo ujenzi ulifikia hatua ya lenta na kupigwa plasta kabla ya Serikali kutoa fedha za kuukamilisha mradi huo.
Kwa upande wake, Dkt. Biteko aliwashukuru wanachama wa CCM na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa fedha za miradi ya maendeleo wilayani Bukombe.
“Niwambie ndugu zangu, maendeleo haya mnayoyaona yanatokana na fedha zinazotolewa na Rais Dkt. Samia. Hivyo tumuombee pamoja na wasaidizi wake ili waendelee kuleta maendeleo nchini na kuijenga Bukombe yetu,” alisema Dkt. Biteko.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Imalanguzu, Mshika Petro, alieleza furaha ya wananchi kwa kupata zahanati hiyo, akisema hapo awali walilazimika kufuata huduma za afya katika vijiji vya mbali.
“Tunamshukuru Mbunge wetu. Kaulimbiu ya kusema na kutenda ameendelea kuiishi, kwani kila alichoahidi amekitekeleza kwa vitendo. Hatuna cha kumlipa zaidi ya kumuunga mkono na kumuombea,” alisema Mshika.
Naye Katibu wa Jumuiya ya Wazazi wa kata hiyo, kwa niaba ya Katibu wa CCM wa Kata, Lameck Igonzela, alisema Ilani ya CCM inaendelea kutekelezwa kwa vitendo kupitia viongozi mbalimbali, akiwemo Diwani, Mbunge na Rais, ambapo miradi ya maendeleo kama barabara, vyumba vinne vya madarasa katika Shule ya Msingi Imalanguzu, pamoja na zahanati hiyo, imefanikishwa.

Comments
Post a Comment