Waziri wa Nishati nchini Tanzania, Deogratius Ndejembi, ametoa maelekezo mazito kwa mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Megawati 49.5 katika maporomoko ya Mto Malagarasi mkoani Kigoma, kufuatia kuchelewesha utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati.
Waziri Ndejembi ametoa kauli hiyo leo Mei 10, 2026 wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo, ambapo alieleza kutoridhishwa na mwenendo wa utekelezaji wa kazi unaofanywa na Kampuni ya Dongfang Electric kutokana na ucheleweshaji wa kazi pamoja na kutotekeleza masharti ya mkataba waliouingia na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Alisema Serikali tayari imelipa zaidi ya dola milioni 20 kama malipo ya awali kwa mkandarasi huyo, lakini kiwango cha kazi zilizotekelezwa hakilingani na fedha zilizotolewa.
Baadhi ya kazi zilizotajwa kuchelewa ni pamoja na ujenzi wa makazi ya wafanyakazi na barabara za mradi, hali iliyoonesha kusuasua kwa utekelezaji wa mradi huo muhimu kwa taifa.
Aidha, Waziri Ndejembi ameielekeza TANESCO pamoja na mshauri mwelekezi kuendelea kumsimamia kwa karibu mkandarasi huyo huku akisisitiza kuwa Serikali haitatoa nyongeza ya fedha wala kuruhusu mabadiliko ya gharama za mradi, kwa kuwa mkandarasi aliwasilisha gharama zake mwenyewe wakati wa zabuni.
Pia ameielekeza TANESCO kukamilisha ukaguzi wa mradi huo ndani ya wiki mbili na kuwasilisha taarifa ofisini kwake.
Alisema baadhi ya wakandarasi wamekuwa wakitumia mbinu ya kuomba kazi kwa gharama ndogo ili kushinda zabuni, kisha baadaye kuanza kuomba nyongeza ya fedha, jambo ambalo Serikali haitalivumilia.
Katika hatua nyingine, Waziri Ndejembi ameagiza meneja wa mradi upande wa mkandarasi kuondolewa mara moja kutokana na kile alichokieleza kuwa ni visingizio vinavyochangia kuchelewesha utekelezaji wa kazi.
Vilevile, ameagiza kufanyika kwa ukaguzi maalum wa matumizi ya fedha za malipo ya awali ili kubaini namna fedha hizo zimetumika ukilinganisha na kazi zilizotekelezwa.
“Mradi huu una umuhimu mkubwa kwa wananchi wa Kigoma, Katavi, Kagera na maeneo ya jirani kwani utaongeza nguvu katika Gridi ya Taifa na kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini. Serikali haitakuwa tayari kuvumilia ucheleweshaji unaosababishwa na uzembe wa wakandarasi,” alisema Waziri Ndejembi.
Aidha, amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, kwa juhudi za kufanya vikao vya mara kwa mara na mkandarasi huyo pamoja na kuchukua hatua mbalimbali za kutatua changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa mradi.
Kwa upande wake, Twange alisema TANESCO imepokea maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri na itahakikisha yanatekelezwa kwa wakati ili mradi huo ukamilike kama ilivyopangwa.
Alisema Mradi wa Malagarasi MW 49.5 unatekelezwa na Kampuni ya Dongfang Electric International Corporation (DEC) kutoka China, ambapo utekelezaji wake ulianza Aprili 30, 2024 na unatarajiwa kukamilika Oktoba 30, 2027 kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 300.

Comments
Post a Comment