WATALAMU WA AFYA WAMPONGEZA RAIS DKT. SAMIA NA DKT. BITEKO KWA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA NAMONGE

Na, Ernest Magashi

Wataalamu wa afya katika Kituo cha Afya Namonge, kilichopo Kata ya Namonge Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuboresha sekta ya afya kupitia ujenzi wa miundombinu, kuongeza watumishi pamoja na upatikanaji wa gari la kubeba wagonjwa (ambulance).Shukrani hizo zilitolewa na Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Namonge, Dkt. Ezekiel Mollel, kwa niaba ya wataalamu wa afya wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa wa Geita, Lucas Mazinzi, aliyefika kituoni hapo pamoja na viongozi wengine kukabidhi zawadi kwa kinamama waliojifungua katika wodi ya wazazi, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kilele cha Wiki ya Wazazi Mkoa wa Geita yaliyofanyika katika Kata ya Namonge.Dkt. Mollel alisema Kituo cha Afya Namonge kilianza kutoa huduma mwezi Februari mwaka 2021 kikiwa na jengo moja la wagonjwa wa nje na watumishi watano pekee, huku kikihudumia vijiji vinane vya Kata ya Namonge pamoja na baadhi ya vijiji vya kata jirani.

Alisema kwa sasa kituo hicho kina jumla ya watumishi 38, ambapo watumishi 35 wameajiriwa na Serikali, wawili ni kutoka shirika la ICAP na mmoja ni wa kujitolea. Aidha, kituo hicho kina wahudumu wa afya ngazi ya jamii wawili kwa kila kitongoji.Dkt. Mollel alisema pamoja na kumshukuru Rais Dkt. Samia, wataalamu wa afya pia wanampongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa ushirikiano wake mkubwa na Serikali uliowezesha upatikanaji wa majengo, watumishi pamoja na gari la wagonjwa ambalo limekuwa msaada mkubwa katika kuwahisha wagonjwa wanaopewa rufaa, wakiwemo wanaohitaji huduma za upasuaji.

"Tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia pamoja na Mbunge wetu Dkt. Biteko kwa ushirikiano wao mkubwa. Serikali imeboresha miundombinu ya afya, imeongeza watumishi na imetoa gari la wagonjwa ambalo limeimarisha huduma kwa wananchi," alisema Dkt. Mollel.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mollel alimshukuru Diwani wa Kata ya Namonge, Mlalu Bundala, kwa kuendelea kushirikiana na watumishi wa kituo hicho, jambo ambalo limechangia kuwepo kwa mazingira mazuri ya kazi.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Namonge, Mlalu Bundala, alisema maendeleo hayo yametokana na uwepo wa Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kutatua changamoto za wananchi.Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Bukombe, Hassan Mohamed, aliwapongeza wauguzi kwa huduma bora wanazotoa, hususan kwa mama na mtoto, akieleza kuwa tangu walipofika katika kituo hicho hawajapokea malalamiko kutoka kwa wananchi.

Mohamed aliwataka wataalamu wa afya kuendelea kutunza na kulinda miundombinu inayojengwa na Serikali kwa manufaa ya wananchi.

Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi kwa kinamama waliojifungua, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa wa Geita, Lucas Mazinzi, aliwapongeza wataalamu wa afya kwa kazi nzuri wanayoifanya na kueleza kuwa Serikali ya Rais Dkt. Samia inaendelea kuleta maendeleo makubwa nchini ikiwemo kuboresha huduma za afya.Mazinzi alisema Dkt. Doto Biteko ni mbunge mwenye ushirikiano mzuri na Serikali pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM), jambo linalosaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi.Kwa nyakati tofauti, baadhi ya wazazi waliopokea zawadi, akiwemo Retisia Daud, Retisia Saimon na Ephulen Henure, waliishukuru Serikali pamoja na viongozi wa Jumuiya ya Wazazi kwa kuwapatia zawadi na kuwajali.Retisia Daud alisema alifurahishwa na mapokezi mazuri pamoja na huduma bora alizopata hadi kujifungua salama.Naye Retisia Saimon alimpongeza Dkt. Biteko kwa mchango wake katika kuboresha huduma za afya kupitia upatikanaji wa gari la wagonjwa.

Kwa upande wake, Ephulen Henure aliwashukuru viongozi wa Jumuiya ya Wazazi CCM kwa kuwapa zawadi mbalimbali ikiwemo sabuni, akisema msaada huo utawasaidia katika shughuli za usafi na malezi ya watoto wao.

Comments