Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita imetenga shilingi milioni 256 kwa ajili ya utoaji wa mikopo isiyo na riba kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika robo ya nne ya mwaka wa fedha.
Akizungumza wakati wa ziara ya Mbunge wa Jimbo la Bukombe ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Dkt. Doto Biteko, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Erick Kagoma, alisema fedha hizo zitatolewa kwa vikundi vitakavyokidhi vigezo baada ya kufanyiwa tathmini na wataalamu wa halmashauri.
Kagoma aliwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiunga katika vikundi na kuomba mikopo hiyo ili waweze kunufaika nayo na kukuza uchumi wa familia zao. Alibainisha kuwa lengo la mikopo hiyo ni kuwawezesha kiuchumi makundi maalum na kuinua kipato chao.
Aliongeza kuwa mapema mwaka huu, halmashauri ilitoa zaidi ya shilingi milioni 196 kwa vikundi 26, hatua iliyowezesha wanufaika kuanzisha na kuendeleza shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Katika ziara hiyo, Diwani wa Kata ya Bukombe, Rozaria Masokola, akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kata hiyo amabo waliungana pamoja na Kata ya Lyambangongo, alimpongeza Mbunge Dkt. Biteko kwa juhudi zake katika kuleta maendeleo, akieleza kuwa utekelezaji wa miradi unaendelea vizuri kutokana na upatikanaji wa fedha za serikali.
Kwa upande wake, Dkt. Biteko aliwataka wananchi na wanachama wa CCM kutumia fursa ya mikopo hiyo isiyo na riba ili kubadili maisha yao. Pia alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
“Niwambie ndugu zangu wanachama na wananchi, maendeleo mnayoyaona Bukombe yanatokana na juhudi za Rais Dkt. Samia. Ni vyema tuendelee kumuunga mkono na kumuombea ili aendelee kutuletea maendeleo,” alisema Dkt. Biteko.
Alisisitiza kuwa Halmashauri ya Bukombe ni miongoni mwa halmashauri zinazoongoza kwa utoaji wa mikopo isiyo na riba kwa makundi hayo, na hivyo kuwataka wananchi kuitumia fursa hiyo kuboresha maisha yao.
Aidha, Dkt. Biteko alisema ana deni kwa wananchi la kutekeleza ahadi alizotoa wakati wa kampeni, akiahidi kuwa ataendelea kusimamia utekelezaji wake kikamilifu. Alitoa wito wa umoja na ushirikiano miongoni mwa wananchi, akieleza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana bila mshikamano na kujitoa kwa pamoja.

Comments
Post a Comment