Wananchi wa Kijiji cha Nyamagwangala, Kata ya Namonge, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wamempongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu mstafu, Dkt. Doto Biteko, kwa kuunga mkono jitihada za wananchi katika ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho hadi kufikia hatua ya kuezeka pamoja na kukamilisha jamvi.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyamagwangala 'A', Patrick Magenga, alisema ushirikiano uliopo kati ya wananchi na Mbunge wao umechangia kufanikisha hatua hiyo muhimu ya maendeleo.
Magenga alisema Dkt. Biteko aliwasikiliza wananchi kuhusu changamoto zao na kubaini kuwa kipaumbele chao kikubwa kilikuwa ni ujenzi wa zahanati, jambo lililomfanya kuhamasisha ujenzi huo kwa kushirikiana na wananchi hatua kwa hatua.
Alisema kabla ya ujenzi huo, wananchi walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya, hali iliyowalazimu kuchangishana fedha ili kupata huduma hizo kutokana na changamoto ya umbali.
Aidha, alisema zahanati hiyo ikikamilika na kuanza kutoa huduma, itawapunguzia wananchi adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Kijiji cha Bwenda, Musa Lutama, alisema ujenzi huo umefikia hatua za mwisho ambapo kinachoendelea ni ukamilishaji wa vyoo ili zahanati hiyo iweze kuanza kutoa huduma rasmi.
Lutama alisema wananchi wanamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa fedha zilizotolewa kukamilisha mradi huo, huku wakiahidi kuendelea kumuombea pamoja na Dkt. Biteko.
Naye Diwani wa Kata ya Namonge, Mlalu Maziku, alisema hatua iliyofikiwa katika ujenzi huo ni matokeo ya ufuatiliaji wa karibu uliofanywa na Mbunge Dkt. Biteko ambaye tangu mwanzo ameendelea kuunga mkono nguvu za wananchi.
Alisema wananchi pia wanamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa shilingi milioni 50 zitakazosaidia kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo.
Maziku alisema kabla ya mwaka 2015, kata hiyo haikuwa na kituo chochote cha kutolea huduma za afya, lakini kwa sasa kuna zahanati nne katika vijiji vya Bwenda, Ilyamchele, Namalandula na Nasiluluma, pamoja na Kituo cha Afya Namonge ambacho Serikali kwa kushirikiana na Mbunge imewezesha kupatikana kwa gari la kubebea wagonjwa.
"Hata vijiji vya Shilabela, Bugege na Mji Mwema ambavyo bado havina zahanati, ujenzi wake unaendelea katika hatua mbalimbali. Tunamshukuru sana Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, ambaye amekuwa mstari wa mbele kutuunga mkono na kufuatilia fedha za ukamilishaji wa miradi ya maendeleo," alisema Bundala.
Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa manufaa ya jamii nzima.

Comments
Post a Comment