WANACHAMA WA CCM WAMPOGEZA DKT. BITEKO KWA KUENDELEZA MIRADI YA MAENDELEO


Na, Ernest Magashi

Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kata za Bukombe na Lyambamgongo, wilayani Bukombe mkoani Geita, wamempongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Dkt. Doto Biteko, kwa juhudi zake za kusukuma maendeleo na kutatua changamoto za wananchi.Pongezi hizo zilitolewa na Diwani wa Kata ya Bukombe, Rozaria Masokola, wakati wa ziara ya Dkt. Biteko ya kuwashukuru wanachama. Alisema mbunge huyo amekuwa mstari wa mbele katika kuleta maendeleo, akibainisha kuwa zaidi ya shilingi milioni 120 zimetolewa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa zahanati tatu, ikiwemo ya Nasihukulu na Imalanguzu, ambazo zilianzishwa kwa nguvu za wananchi kwa kushirikiana na mbunge huyo.Masokola alieleza kuwa kukamilika kwa zahanati hizo kutapunguza changamoto ya wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya. Aidha, alibainisha kuwa vitongoji vyote vya Kata ya Bukombe vinatarajiwa kupata umeme kupitia mradi wa REA, jambo linaloonesha dhamira ya mbunge katika kuboresha maisha ya wananchi.Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma, alimpongeza Dkt. Biteko kwa kuendelea kushirikiana na viongozi wa CCM na wananchi katika kuharakisha maendeleo katika kata mbalimbali za wilaya hiyo.Akizungumza kuhusu miradi ya maendeleo, Dkt. Biteko alisema fedha zinazotekeleza miradi hiyo zinatolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambae nampongeza sana mbele yenu kwa lengo la kuibadirisha Wilaya ya Bukombe. Alitaja baadhi ya miradi iliyotekelezwa kuwa ni pamoja na ujenzi wa zahanati za Kagwe na Lyambamgongo, uboreshaji wa mtandao wa barabara ikiwemo barabara za Lyambamgongo, Kagwe, Lyambamgongo na Ifunde hadi Maganzo, pamoja na Lyambamgongo hadi Nyamakunkwa. Pia alieleza kuwa usambazaji wa umeme katika vitongoji unaendelea.“Ninawashukuru sana wanachama wa CCM kwa kumchagua Rais Samia, mimi pamoja na madiwani. Nawahakikishia kuwa ahadi tulizotoa wakati wa kampeni tutazitekeleza. Naomba muendelee kuyasema mazuri yanayofanywa na Rais Samia,” alisema Dkt. Biteko.Aidha, alisisitiza umuhimu wa umoja na upendo miongoni mwa wananchi, huku akieleza mafanikio makubwa yaliyopatikana Bukombe, ikiwemo ujenzi wa barabara ya lami kutoka Ushirombo hadi Katoro, ujenzi wa uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu, soko jipya na stendi ya mabasi, pamoja na ongezeko la shule za sekondari za kidato cha tano na sita kutoka moja hadi tano kwa sasa.Aliongeza kuwa kila tarafa sasa ina shule ya kidato cha tano na sita, huku akibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuleta fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya afya, maji na barabara, ambapo mtandao wa barabara umeongezeka kutoka kilomita 256 hadi zaidi ya kilomita 1,500, zikiwemo barabara za lami katika miji ya Ushirombo na Runzewe.Katika ziara hiyo, Dkt. Biteko aliambatana na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukombe, Kihanda Lutonja, pamoja na wajumbe wa Kamati ya Siasa ya wilaya. Lutonja alimpongeza mbunge huyo kwa kuanza ziara ya kuwashukuru wanachama ndani ya chama kabla ya kuanza mikutano ya hadhara kwa wananchi.

Comments