Zoezi la uokoaji limeanza kufuatia watu watatu kudaiwa kufukiwa na kifusi cha mchanga katika Mgodi wa Madukajohn & Partners uliopo kijiji cha Kelezia, Kata ya Igulwa, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita.
Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja wa mgodi huo, Peter Joseph, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa juhudi za uokoaji zimeanza rasmi leo Mei 29, 2026 kwa kushirikiana na vyombo vya dola, jeshi la zimamoto na uokoaji pamoja na wataalamu kutoka ofisi ya madini.
Joseph alisema tukio hilo lilitokea Mei 28, 2026 majira ya saa 9:00 alasiri, wakati watu hao watatu walipoingia kwenye duwara namba 20 “B” kwa ajili ya kufanya ukarabati wa kufunga matimba kufuatia maelekezo ya wakaguzi wa mgodi.
Aliwataja waliofukiwa kuwa ni Renad Charles (29) na Juma Hussen (27), wakazi wa Masumbwe, pamoja na Ave Mchele (37), mkazi wa mtaa wa Kalole Mbogwe, ambao wote ni mafundi wa kufunga matimba mgodini hapo.
Joseph alieleza kuwa eneo hilo lilikuwa limezuiwa kuendelea kufanyiwa kazi na wakaguzi wa migodi ili kupisha ukarabati. Aliongeza kuwa tangu mgodi huo uanze kufanya kazi mwaka 2024, haijawahi kutokea tukio kubwa la watu kufukiwa, licha ya kuwepo matukio ya majeruhi wakati wa kazi.
“Tunamuomba Mungu wenzetu waweze kuokolewa wakiwa hai kwani walikuwa katika shughuli za utafutaji ndani ya mgodi,” alisema Joseph.
Diwani wa Kata ya Igulwa, Richard Mabenga, aliyefika eneo la tukio, alimshukuru Mkuu wa Wilaya ya Bukombe kwa kupeleka vyombo vya dola kushirikiana na wataalamu wa madini pamoja na jeshi la uokoaji katika juhudi zinazoendelea.
Mabenga pia alitoa pole kwa ndugu na jamaa wa waliofukiwa, wachimbaji, mafundi wa kufunga matimba pamoja na wananchi wanaozunguka mgodi huo ambao wamekusanyika kusubiri matokeo ya uokoaji.
Kwa upande wake, fundi wa kufunga matimba, Mawazo Paul, aliyekuwa eneo la tukio kabla ya ajali hiyo, alisema alikuwa pamoja na mafundi hao akifanya kazi kabla hajatoka kwenda kuwapelekea maji wenzake, muda mfupi kabla kifusi hakijaanguka.
“Nilitoka kuwafuatia maji, ndipo muda mfupi baadaye kifusi kikaanguka na kuwafukia wenzangu watatu,” alisema Mawazo.

Comments
Post a Comment