UKUSANYAJI WA MAPATO YA NDANI WAFIKIA ASILIMIA 109 BUKOMBE


Na, Ernest Magashi

Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita imefanikiwa kufikia asilimia 109 ya ukusanyaji wa mapato ya ndani hadi kufikia Mei 1, 2026, hatua inayotajwa kuwa mafanikio makubwa katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo.Mafanikio hayo yalielezwa na Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Paskasi Muragili, wakati akitoa pongezi kwa Madiwani pamoja na wataalamu wa Halmashauri hiyo kwa ushirikiano wao mzuri uliochangia kuongezeka kwa mapato kabla ya kuhitimishwa kwa mwaka wa fedha 2025/2026.Akizungumza katika Baraza la Madiwani, Mhandisi Muragili alisema katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026, Halmashauri imeendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali kwa kusimamia ukusanyaji wa mapato kwa ufanisi, hali inayotoa matumaini ya kuvuka lengo lililowekwa.“Mafanikio haya yanaonesha kuwa Halmashauri imefikia na hata kuvuka malengo ya ukusanyaji wa mapato, jambo linaloleta matumaini makubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma bora kwa wananchi,” alisema Mhandisi Muragili.Aidha, aliwapongeza wataalamu na Madiwani kwa kazi nzuri wanayoifanya huku akiwasisitiza kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha malengo ya maendeleo yanafikiwa.Katika kuhakikisha wananchi wanapata nafasi ya kusikilizwa na kutatuliwa changamoto zao, Mkuu huyo wa Wilaya aliliagiza Baraza la Madiwani kwa kushirikiana na Mkurugenzi Mtendaji pamoja na wataalamu wengine kuendelea kufanya vikao vya kusikiliza na kutatua kero katika kila kijiji. Pia aliwataka Madiwani kuwa mstari wa mbele katika zoezi hilo.Kwa upande mwingine, Mhandisi Muragili aliwataka wafugaji kutenga maeneo maalum ya malisho pamoja na kulima nyasi kwa ajili ya mifugo yao ili kuepusha mifugo kuingia kwenye mashamba ya wakulima na kusababisha migogoro kati ya wakulima na wafugaji.Kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo, alisema Serikali itaendelea kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa inakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma stahiki kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Adelina Mfikwa, alisema watumishi wa Halmashauri wataendelea kutoa ushirikiano kwa Madiwani kama ambavyo wamekuwa wakishirikiana katika utekelezaji wa shughuli za ukusanyaji mapato.Mfikwa alisema licha ya mafanikio katika ukusanyaji wa mapato, Halmashauri imeanza kufanya mikutano ya hadhara kwa kushirikiana na wataalamu hadi ngazi ya vijiji kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi.Alisema mikutano hiyo itaendelea kufanyika kwa kushirikiana na watumishi wa kada mbalimbali, wakiwemo maafisa wanaosimamia utawala bora.Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukombe, Matondo Lutonja, aliwapongeza Madiwani pamoja na wataalamu kwa kuvuka malengo ya ukusanyaji wa mapato ya ndani.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma, alisema Madiwani wamejipanga kuendelea kushirikiana na wataalamu ili kuhakikisha malengo ya maendeleo yanafikiwa.

“Niwaombe wataalamu wa idara zote za Serikali, wakiwemo polisi, tushirikiane kwa kila hatua ili kufikia malengo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea maendeleo wananchi. Pia tuendelee kuishi katika kauli ambayo imekuwa ikitumiwa na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwamba kila mmoja amfanye mwenzake afurahi,” alisema Kagoma.

Comments