Operesheni ya uokoaji wa watu watatu wanaodaiwa kufukiwa na kifusi cha mchanga katika mgodi wa Madukajohn & Patinas uliopo Kijiji cha Kelezia, Kata ya Igulwa, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, imeingia siku ya pili huku juhudi za kufukua zikiendelea.
Ndugu na jamaa wa watu hao wameendelea kufika eneo la tukio wakisubiri kwa matumaini kuona ndugu zao wanaokolewa.Meneja wa mgodi huo, Peter Joseph, alisema kuwa kazi ya kuondoa kifusi kilichoanguka inaendelea kwa ushirikiano wa vyombo vya dola, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na wataalamu kutoka Ofisi ya Madini.
Alisema operesheni hiyo ilianza Mei 29, 2026 kufuatia tukio lililotokea Mei 28, 2026 majira ya saa 9:00 alasiri, ambapo watu hao walikuwa ndani ya duwara namba 20 "B" wakifanya kazi ya kufunga matimba kwa mujibu wa maelekezo ya wakaguzi wa mgodi.
Joseph aliwataja watu wanaodaiwa kufukiwa kuwa ni Renad Charles (29) na Juma Hussein (27), wote wakazi wa Masumbwe, pamoja na Ave Mchele (37), mkazi wa Kalole, Wilaya ya Mbogwe. Wote ni mafundi wa kufunga matimba mgodini.
Baadhi ya ndugu wa waliofukiwa, akiwemo Merina Wilson na Ernest Manyama, wamepongeza juhudi zinazofanywa na uongozi wa mgodi pamoja na vyombo vya dola katika kuendelea na operesheni ya uokoaji.
Hata hivyo, wameiomba Serikali kuongeza nguvu katika shughuli hiyo kwa kupeleka mitambo ya kisasa ya kufukua kifusi ili kuharakisha zoezi la uokoaji, wakieleza kuwa matumizi ya nguvu kazi ya mikono pekee yanafanya operesheni hiyo kwenda kwa kasi ndogo.
Merina Wilson, ambaye ni mke wa Juma Hussein, alisema kabla ya tukio hilo waliamka salama na kwenda kwenye majukumu kwa amani kila mmoja akielekea kwenye shughuli zake za kila siku.
Alisema baada ya kupata taarifa za tukio hilo alifika eneo la mgodi na kukuta watu wengi wakiwa wamekusanyika, ndipo alipothibitishiwa kuwa mume wake alikuwa miongoni mwa waliofukiwa.
"Naomba Serikali iongeze nguvu kwa kuleta mtambo wa kufukua ili zoezi liweze kwenda haraka zaidi. Leo ni siku ya pili na tunaendelea kusubiri kwa matumaini makubwa," alisema Merina.
Kwa upande wake, ndugu mwingine, Peter Jackson, alisema hatua zinazoendelea ni nzuri licha ya kuwa za taratibu, huku akiitaka Serikali kuendelea kufuatilia kwa karibu operesheni hiyo na kutafuta njia za kuongeza kasi ya uokoaji.
Naye Diwani wa Kata ya Igulwa, Richard Mabenga, amewaomba ndugu wa watu wanaodaiwa kufukiwa kuwa na subira wakati vyombo husika vikiendelea na juhudi za kuwaokoa.
Alisema Serikali inafuatilia kwa karibu tukio hilo na kwamba operesheni ya uokoaji inaendelea chini ya usimamizi wa vyombo vya dola, ikiwemo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

Comments
Post a Comment