SERIKALI YATOA SIKU TATU KWA WACHIMBAJI NA WANUNUZI KUWASILISHA CHANGAMOTO ZAO ILI ZIPATIWE UFUMBUZI

Na, Ernest Magashi

Serikali imetoa siku tatu kwa wachimbaji na wanunuzi wa madini ya jasi kuwasilisha mchanganuo wa gharama za uzalishaji pamoja na changamoto zinazowakabili, ili kufanikisha upatikanaji wa suluhisho litakalowanufaisha wadau wote wa sekta hiyo.Agizo hilo limetolewa leo Mei 14, 2026 jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, wakati akizungumza katika kikao kilichowakutanisha wachimbaji wa madini ya jasi, wanunuzi, kampuni za saruji pamoja na wazalishaji wa gypsum. Kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa Makao Makuu ya Tume ya Madini.Dkt. Kiruswa alisema Serikali inahitaji kila upande kuwasilisha kwa kina changamoto zake ili kufanya uchambuzi utakaowezesha kupatikana kwa muafaka wenye manufaa kwa wachimbaji, wanunuzi na watumiaji wa mwisho.

“Tunataka kila upande uainishe mambo yanayouumiza upande mmoja na yanayoubeba upande mwingine, ili baada ya uchambuzi huo tupate suluhisho la pamoja,” alisema Dkt. Kiruswa.Aidha, alisema Serikali itafanyia kazi malalamiko kuhusu tozo mbalimbali zinazotozwa na baadhi ya halmashauri, ambazo zimeelezwa kuongeza gharama za uzalishaji na biashara ya madini ya jasi.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo wa Madini ya Jasi Mkoa wa Lindi, Salum Kassim, alisema bei ya madini hayo haijawahi kuongezeka tangu mwaka 2016 licha ya kupanda kwa gharama za uzalishaji, zikiwemo mafuta, vipuri vya mitambo na mishahara ya wafanyakazi.Alisema hali hiyo imeathiri uzalishaji na kusababisha wachimbaji wengi kushindwa kupata faida katika biashara hiyo.Katika mapendekezo yao, wachimbaji wamependekeza bei ya tani moja ya jasi kwa maeneo ya Dar es Salaam na Pwani iongezwe kutoka shilingi 110,000 hadi 150,000. Kwa Mkoa wa Mtwara, bei ipande kutoka shilingi 75,000 hadi 95,000, huku Mkuranga ikipendekezwa kuongezeka kutoka shilingi 95,000 hadi 130,000. Aidha, eneo la Kiranjeranje bei imependekezwa kuongezeka kutoka shilingi 60,000 hadi 75,000 kwa tani.Kwa mujibu wa Kassim, marekebisho hayo ya bei yatasaidia kufufua uzalishaji wa madini ya jasi na kuboresha maisha ya wachimbaji ambao kwa sasa wanakabiliwa na changamoto kubwa za uendeshaji.Naye Mkurugenzi wa Manunuzi wa Dangote Cement Limited⁠, Halima Kuchwa, alitoa tahadhari kuwa ongezeko la gharama za malighafi linaweza kuathiri bei ya saruji sokoni na hatimaye kumgusa mtumiaji wa mwisho.

Kuchwa alisema madini ya jasi ni miongoni mwa malighafi muhimu inayotumika katika uzalishaji wa saruji, gypsum na bidhaa nyingine za ujenzi nchini. Tanzania ina maeneo kadhaa yenye uzalishaji wa jasi, ikiwemo Lindi, Mtwara, Pwani na Mkuranga.Kwa miaka ya hivi karibuni, wachimbaji wadogo wamekuwa wakilalamikia kupanda kwa gharama za uzalishaji huku bei ya soko ikibaki ileile kwa muda mrefu, hali inayodaiwa kupunguza tija na kuathiri uzalishaji wa madini hayo.

Comments