SERIKALI KUAJIRI WAUGUZI WAPYA 165 BUKOMBE MWAKA HUU


Na, Ernest Magashi

ebukombesasa.blogspot.com.tz

Serikali inatarajia kuajiri wauguzi wapya 165 katika Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kukabiliana na changamoto ya upungufu wa watumishi wa afya na kuboresha huduma za afya kwa wananchi.Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Paskas Muragili, wakati akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani yaliyofanyika kiwilaya wilaya Bukombe Mei 22, 2026, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela.Mhandisi Muragili alisema Serikali tayari imeanza kushughulikia changamoto ya upungufu wa wauguzi iliyowasilishwa na Chama cha Wauguzi Wilaya ya Bukombe, ambapo hadi sasa wauguzi 98 tayari wamesharipoti kazini wilayani humo huku wengine 165 wakitarajiwa kuajiriwa kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha. Aidha, wauguzi 18 wanaendelea na masomo yao.Aliwahakikishia wauguzi kuwa Serikali itaendelea kujenga zahanati, vituo vya afya pamoja na nyumba za watumishi katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu na vyombo vya ulinzi na usalama."Tunatambua umuhimu wa wauguzi kwa kuwa wao ndio hutumia muda mwingi zaidi na wagonjwa. Tunawapongeza kwa kazi kubwa mnayoifanya kwani hakuna malalamiko makubwa kutoka kwa wananchi kuhusu huduma zenu. Serikali inaendelea kuhakikisha huduma za afya zinatolewa kwa ubora unaostahili," alisema Mhandisi Muragili.Akitoa salamu za Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu mstaafu Dkt. Doto Biteko, Mkuu huyo wa Wilaya alisema Dkt. Biteko amekuwa mstari wa mbele katika kuwajali na kuwasikiliza wauguzi pamoja na watumishi wa kada mbalimbali."Dkt. Biteko amewapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuhudumia wananchi na amesisitiza muendelee kudumisha umoja, upendo na ushirikiano katika kazi zenu," alisema Muragili.Aidha alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kupeleka fedha nyingi za maendeleo hususan katika sekta ya afya, jambo lililowezesha ujenzi wa zahanati na vituo vya afya kuazia ngazi ya vijijini.Awali, Katibu wa Chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA) Wilaya ya Bukombe, Leodgard Marco, alisema maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kaulimbiu isemayo: "Wauguzi Wetu, Mustakabali Wetu: Wauguzi Waliowezeshwa Huokoa Maisha."Marco aliipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha mazingira ya kutolea huduma za afya kupitia ujenzi wa vituo vya afya, ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa pamoja na utoaji wa ajira kwa watumishi wa afya.Alisema vifaa vya kisasa vimeongeza ufanisi wa utoaji wa huduma huku vikiboresha mazingira ya kazi kwa wauguzi na wagonjwa.Marco alisema Wilaya ya Bukombe ina jumla ya wauguzi 310, ambapo kati yao 230 wanahudumu katika vituo vya Serikali huku wauguzi 80 wakifanya kazi katika vituo binafsi na vya mashirika ya kidini.Hata hivyo alisema bado kuna upungufu wa wauguzi katika baadhi ya vituo vya kutolea huduma za afya jambo linalochangia wagonjwa kutumia muda mrefu kusubiri huduma."Tunaiomba Serikali iendelee kuajiri wauguzi sambamba na ongezeko la vituo vya kutolea huduma za afya," alisema Marco.Kwa upande wake, Muuguzi Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Diana Makubi, alisema ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wagonjwa wameanzisha madawati ya kupokea na kusikiliza changamoto za wateja katika vituo vya afya.Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Adelina Mfikwa, aliwapongeza wauguzi kwa kazi yao na kuwataka kuendelea kushirikiana ili wananchi waendelee kupata huduma bora.Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma, alisema changamoto zilizowasilishwa na wauguzi zitafanyiwa kazi kwa kutambua mchango wao mkubwa katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Comments