MAZINZI AHAMASISHA UPANDAJI MITI NA UTUNZAJI WA MAZINGIRA


Na, Ernest Magashi

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa wa Geita, Lucas Mazinzi, amewataka wananchi kuendelea kupanda miti ya vivuli, matunda na mbao ili kusaidia utunzaji wa mazingira pamoja na kukuza uchumi wa familia.Wito huo aliutoa wakati akizungumza na wananchi pamoja na walimu baada ya kushiriki zoezi la upandaji miti katika Shule ya Msingi Dkt. Samia Suluhu iliyopo Kata ya Namonge, Wilaya ya Bukombe, katika maadhimisho ya Siku ya Jumuiya ya Wazazi CCM Kimkoa.Akiwa shuleni hapo, Mazinzi aliwataka walimu kuendelea kushirikiana na wazazi pamoja na walezi katika kuwapatia wanafunzi malezi bora na maadili mema. Pia alisisitiza umuhimu wa kutunza mazingira ya shule kwa kupanda na kuhifadhi miti pamoja na kulinda miundombinu iliyojengwa kwa gharama kubwa na Serikali.Kwa upande wake, Mwalimu wa somo la Jiografia na utunzaji wa mazingira katika Shule ya Msingi Dkt. Samia Suluhu, Lenard Batali, aliahidi kuwa miti iliyopandwa na viongozi wa Jumuiya ya Wazazi CCM ngazi ya Wilaya na Mkoa itatunzwa vizuri ili iweze kuwanufaisha wanafunzi kwa kuwapatia kivuli wakati wa mapumziko na wanapokuwa darasani."Tunashukuru sana kwa kuitembelea shule yetu na kuja na miti ambayo imepandwa hapa shuleni. Hakika miti hii itasaidia kwa kiasi kikubwa katika utunzaji wa mazingira, na tunaahidi kuitunza kwa umakini mkubwa," alisema Mwalimu Batali.Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Bukombe, Hassan Mohamed, aliwaomba walimu kushirikiana na wanafunzi katika kuhakikisha miti iliyopandwa na viongozi inadumu na kuwanufaisha wanafunzi, jambo ambalo litasaidia kuifanya shule kuwa na mazingira bora na yenye mvuto zaidi.

Comments