MATONE YA POLIO AWAMU YA PILI KUFIKIA WATOTO 189,253 BUKOMBE


Na, Ernest Magashi

Chanjo ya matone dhidi ya ugonjwa wa Polio, unaoweza kusababisha ulemavu wa kudumu, inatarajiwa kuanza kwa awamu ya pili katika Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita.Akizungumza katika kikao cha wadau wa afya na viongozi wenye ushawishi katika jamii, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Paskasi Muragili, aliwataka washiriki hao kuwa mabalozi wa kuhakikisha watoto wote wanapatiwa chanjo hiyo muhimu.

Mhandisi Muragili alisisitiza kuwa ushiriki wa kila mdau ni nguzo muhimu katika kufanikisha azma ya kuwafikia watoto wote wilayani humo.“Chanjo ya Polio ni salama, yenye ufanisi, na ni haki ya kila mtoto kuipata,” alisema.

Aliongeza kuwa watoto wote wenye umri chini ya miaka 10 wanapaswa kuchanjwa, bila kujali kama waliwahi kupata chanjo hiyo kupitia kliniki au kampeni zilizopita.

“Ni wajibu wetu kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa chanjo. Tuwe mabalozi wa kweli katika jamii zetu ili kufikia kila kaya na kumkinga kila mtoto dhidi ya Polio,” alisisitiza.Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Adelina Mfikwa, alisema kikao hicho kililenga kuongeza uelewa kwa wadau kuhusu ugonjwa wa Polio, umuhimu wa chanjo ya matone na faida zake kwa afya ya mtoto.

Alibainisha kuwa uhamasishaji sahihi utachangia mafanikio ya kampeni hiyo kwa kufikia asilimia 100 ya walengwa.Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Dkt. Deograsia Mkapa, alisema kampeni hiyo ni awamu ya pili ya utoaji wa chanjo ya Polio kwa njia ya matone, itakayofanyika kuanzia Mei 7 hadi 10, 2026.Alieleza kuwa jumla ya watoto 189,253 wanatarajiwa kufikiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe.

Dkt. Mkapa aliwataka wazazi na walezi kujitokeza kwa wingi kuwapeleka watoto wao kupata chanjo hiyo, akisisitiza kuwa ni rahisi kutolewa, haina madhara, na inalinda afya ya mtoto pamoja na jamii kwa ujumla.Aliongeza kuwa kampeni hii ya kitaifa inaendeshwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI pamoja na wadau wa maendeleo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kutokomeza kabisa ugonjwa wa Polio nchini.


Comments