Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wameipongeza Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kazi kubwa ya kufungua mtandao mpya wa barabara mjini na vijijini pamoja na utekelezaji wa miradi ya makaravati, licha ya kuwepo kwa changamoto ndogondogo katika baadhi ya maeneo.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wikaya ya Bukombe Adelina Mfikwa alimuomba meneja wa TARURA Wilaya kusikikiza changamoto zinazo tolewa na madiwani na kuzijibu licha ya kupongezwa.
Pongezi hizo zimetolewa na madiwani mbalimbali wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani walipokuwa wakijadili taarifa ya TARURA.Diwani wa Kata ya Ng’anzo, Mashaka Shing’wenda, aliipongeza TARURA kwa juhudi zake na kuomba barabara za Mtinga, Kazibizyo na Segwe ziboreshewe.
Naye Diwani wa Kata ya Ushirombo, Lameck Warangi, alimpongeza Meneja wa TARURA kwa kazi nzuri anayofanya na kumshauri kuwabana wakandarasi ili kuhakikisha makaravati yanafukiwa kwa wakati.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Katente, Paul Ng’wani, alimpongeza Meneja huyo na kueleza kuwa baadhi ya barabara katika kata yake hazina miundombinu ya kupitisha maji, hali inayosababisha maji kutwama hasa katika maeneo ya mjini.
Aidha, Diwani wa Kata ya Igulwa, Richard Mabenga, aliomba TARURA kuiangalia kwa karibu barabara ya Mtaa wa Magorofani ambako kuna maporomoko ya maji yanayohatarisha miundombinu ya barabara na usalama wa wananchi.
Diwani wa Kata ya Bugelenga, Leonard Lubigisa, alisema utekelezaji wa miradi ya barabara katika kata yake unaendelea vizuri na changamoto kubwa iliyopo ni mvua zinazoathiri kazi za ujenzi. Pia aliomba barabara ya Bugelenga Ikalanga itengenezwe.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma, akiungana na madiwani wengine kuipongeza TARURA, alimtaka Meneja wa TARURA kuhakikisha miradi ya barabara inasimamiwa kwa kuzingatia sheria pamoja na kudhibiti magari yenye uzito mkubwa kupita katika barabara zisizoruhusiwa.
Kagoma alisema baadhi ya barabara kisheria zinapaswa kupitisha magari yenye uzito usiozidi tani 10, lakini baadhi ya wamiliki wa magari wamekuwa wakipitisha magari yenye tani 20 hadi 30, jambo linalosababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ya barabara.
Alisisitiza kuwa sheria za barabara zisimamiwe kikamilifu ili Serikali isilazimike kutumia gharama kubwa za matengenezo kila mwaka kutokana na uharibifu unaoweza kuzuilika.
Pia alimtaka mkandarasi kuleta mitambo na kuendelea na kazi kwa haraka ili kuwaondolea wananchi adha ya usafiri na usafirishaji wa mazao yao.
Akijibu hoja na kupokea pongezi za madiwani, Meneja wa TARURA Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Msoka Msumba, alisema kwa mwaka wa fedha unaokujaa TARURA imesajili barabara mpya 40 zenye urefu wa kilomita 161.672 kwa ajili ya utekelezaji wilayani humo.
Mhandisi Msumba alisema miradi hiyo inahusisha barabara za mjini na vijijini, huku mkandarasi mmoja akitekeleza kazi mbalimbali ikiwemo barabara ya Lyambamgongo kuelekea Nyakagwe ambayo tayari imekamilika.
Akizungumzia changamoto ya maji kutokuwa na njia na kusababisha kutwama kwenye barabara, alisema hali hiyo imetokana na mkandarasi kusubiri wataalamu wa TANROADS kuonyesha maeneo sahihi ya kuchimba mitaro ya kupitisha maji hasa kipindi cha masika.
Alieleza kuwa tayari mitaro imejengwa na mkandarasi anatarajiwa kupeleka mitambo kwa ajili ya kufukia makaravati yote yaliyotajwa na madiwani, huku changamoto kubwa ikiendelea kuwa mvua zinazosababisha mitambo kuzama maeneo yenye matope.
Mhandisi Msumba pia alisema barabara ya Namonge Ilyamchele ina changamoto ya matuta na eneo kubwa la mabondeni, lakini kupitia bajeti ya mwaka wa fedha ujao itafanyiwa maboresho makubwa.
Kupitia Baraza hilo, Meneja huyo wa TARURA aliwaomba madiwani na wadau wa barabara kuendelea kuwaelimisha wananchi kuacha kulima karibu na makaravati kwani hali hiyo husababisha maji kuziba njia zake wakati wa mvua.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Paskasi Muragili, aliungana na madiwani kuipongeza TARURA kwa kazi inayofanya na kueleza kuwa changamoto za wakandarasi anazifahamu na Serikali itaendelea kuzifanyia kazi.
Mhadisi Muragili pia alisisitiza kuwa Meneja wa TARURA apewe ushirikiano ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria, huku akihimiza wadau wote kuheshimu taratibu na sheria zinazolinda utekelezaji wa miradi ya barabara.

Comments
Post a Comment