Madaktari bingwa wa macho kutoka Hospitali ya Mkoa wa Geita pamoja na Hospitali ya Kilimanjaro Christian Medical Centre (KCMC), kwa kushirikiana na wataalamu wa Hospitali ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wameweka kambi maalum ya huduma za afya ya macho katika Kituo cha Afya Uyovu chenye hadhi ya hospitali, kwa lengo la kuwahudumia wananchi wenye changamoto mbalimbali za macho.
Akizungumzia mafanikio ya kambi hiyo, Mratibu wa Afya ya Macho wa Wilaya ya Bukombe, Dkt. Laurent Shelembi, alisema huduma hizo zilitolewa kuanzia Mei 11 hadi Mei 15, 2026 ambapo jumla ya wananchi 245 walipata huduma mbalimbali za afya ya macho kupitia kambi hiyo ya siku tano.
Alisema kuwa kambi hiyo pia iliwezeshwa na mdau wa maendeleo Kilimanjaro Centre for Community Ophthalmology (KCCO) kwa lengo la kuwapatia wananchi huduma za uchunguzi, matibabu na upasuaji wa magonjwa ya macho ili kupunguza tatizo la uoni hafifu na upofu unaoweza kuzuilika.
“Kambi hii imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Bukombe na maeneo ya jirani, kwani wengi wamepata huduma karibu na makazi yao,” alisema Dkt. Shelembi.
Alifafanua kuwa huduma zilizotolewa katika kipindi hicho ni pamoja na uchunguzi wa macho, ushauri wa kitaalamu kuhusu afya ya macho, matibabu ya magonjwa ya macho, upasuaji wa mtoto wa jicho, upasuaji mdogo wa macho pamoja na tathmini ya matumizi ya miwani.
Kwa mujibu wa Dkt. Shelembi, kati ya wagonjwa 245 waliopata huduma, wanaume walikuwa 119 huku wanawake wakiwa 126.
Aidha, wagonjwa 46 walifanyiwa upasuaji mbalimbali, ambapo wagonjwa 36 walifanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho na wengine 10 walifanyiwa upasuaji mdogo wa macho.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Dkt. Deograsia Mkapa, alisema mafanikio ya kambi hiyo yamechangia kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kufanya uchunguzi wa macho mapema pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya wataalamu wa afya wa Wilaya ya Bukombe na hospitali za rufaa.
Dkt. Mkapa aliongeza kuwa Kituo cha Afya Uyovu pia kilinufaika kwa kukusanya mapato ya Shilingi milioni 2.288 kutokana na huduma zilizotolewa wakati wa kambi hiyo.
Hata hivyo, wananchi kwa kushirikiana na uongozi wa Kituo cha Afya Uyovu walitoa shukrani kwa madaktari bingwa wa macho kutoka Hospitali ya Mkoa wa Geita na KCMC kwa kujitolea kwao kutoa huduma muhimu kwa wananchi.

Comments
Post a Comment