LIGI YA KNK CUP KUANZA KUTIMUA VUMBI JULAI 1, 2026; DKT. BITEKO AONGOZA KIKAO CHA MAANDALIZI






Na, Ernest Magashi ebukombesasa.blogspot.com.tz

Mbunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita, Dkt. Doto Biteko, leo Mei 22, 2026 ameongoza kikao maalum cha maandalizi ya mashindano ya ligi ya jimbo maarufu kama KNK CUP, ambayo hapo awali ilikuwa ikijulikana kwa jina la Doto Cup.

Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Biteko alisema kuwa mashindano ya KNK CUP yanalenga kuibua na kukuza vipaji vya vijana katika mchezo wa mpira wa miguu, kuimarisha mshikamano wa wananchi pamoja na kuhamasisha ushiriki wa michezo katika jamii kwa kuzingatia kuwa michezo ni afya.Alisema mashindano hayo, ambayo yamekuwa yakifanyika tangu alipochaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Bukombe 2016, yanatarajiwa kuzinduliwa rasmi Julai 1, 2026 na yataendeshwa kwa mfumo wa mtoano kuanzia ngazi ya vijiji, kata na tarafa hadi kupatikana bingwa wa wilaya.

Aidha, alieleza kuwa mashindano hayo yameendelea kuwa chachu ya kuibua vipaji vya vijana wengi, sambamba na kutoa fursa za ajira, burudani na kukuza mshikamano wa jamii ya Bukombe.Dkt. Biteko alisema mshindi wa kwanza atajinyakulia Shilingi milioni 5, mshindi wa pili Shilingi milioni 3, huku mshindi wa tatu shiligi milioini 2 Pia, zawadi mbalimbali zitatolewa katika hatua tofauti za mashindano kuanzia ngazi ya kata hadi tarafa kabla ya kupatikana bingwa wa wilaya.Aliongeza kuwa KNK CUP imeendelea kuwa miongoni mwa matukio makubwa ya michezo katika Jimbo la Bukombe mkoani Geita kutokana na kuvutia ushiriki mkubwa wa vijana, timu mbalimbali pamoja na wadau wa michezo kila mwaka.Kwa nyakati tofauti mjini Ushirombo, baadhi ya wadau wa mpira wa miguu akiwemo Matokeo Kapipi wamempongeza Dkt. Biteko kwa juhudi hizo za kuendelea kuimarisha michezo jimboni humo.

Walisema kuwa kupitia mashindano hayo wananchi wataendelea kupata burudani huku vijana wakipata fursa ya kuonyesha vipaji vyao wakati vumbi la soka litakapoanza kutimuka.

Comments