KASI YA UOKOAJI YAONGEZEKA KATIKA JUHUDI ZA KUWAFIKIA WATU WATATU WALIOFUKIWA NA KIFUSI MGODINI

Na, Ernest Magashi

ebukombesasablogspot.com.tz

Juhudi za uokoaji wa watu watatu wanaodaiwa kufukiwa na kifusi katika Mgodi wa Madukajohn & Patinas uliopo kijiji cha Kelezia kata ya Igulwa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, zinaendelea kwa kasi leo, ikiwa ni siku ya tatu tangu operesheni hiyo ilipoanza Mei 29, 2026.

Akizungumza na waandishi wa habari jioni ya leo Mei 31, 2026, Meneja wa mgodi huo, Peter Joseph, alisema waokoaji wamepiga hatua kubwa katika ufukuaji wa kifusi kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na maofisa kutoka Ofisi ya Madini.“Matumaini yapo ya kuwapata ndugu zetu. Tunaendelea kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha tunawafikia haraka iwezekanavyo. Tunamuomba Mungu tuwakute wakiwa salama, na kufikia kesho tutakuwa tumesonga mbele zaidi katika operesheni hii,” alisema Joseph.Alieleza kuwa operesheni ya uokoaji ilianza Mei 29, 2026 kufuatia tukio la Mei 28, 2026 majira ya saa 9:00 alasiri, ambapo watu hao walifukiwa na kifusi walipokuwa ndani ya duwara namba 20 “B” wakifanya kazi ya kufunga matimba kwa mujibu wa maelekezo ya wakaguzi wa mgodi.

Joseph aliwataja wanaodaiwa kufukiwa kuwa ni Renad Charles (29) na Juma Hussein (27), wote wakazi wa Masumbwe, pamoja na Ave Mchele (37), mkazi wa Kalole, Wilaya ya Mbogwe. Wote ni mafundi wa kufunga matimba mgodini.Baadhi ya ndugu wa waliofukiwa, akiwemo Merina Wilson na Ernest Manyama, wamewaomba Watanzania kuendelea kuwaombea wapendwa wao ili waokoaji watakapowafikia waweze kuwakuta wakiwa hai na salama.Tukio hilo limeendelea kuvuta hisia za wananchi huku wengi wakifuatilia kwa karibu maendeleo ya operesheni ya uokoaji inayofanyika katika mgodi huo.

Comments