DKT. BITEKO AUNGANA NA DC KUWAPONGEZA WATAALAMU NA MADIWANI KWA UKUSANYAJI MAPATO BUKOMBE


Na, Ernest Magashi

Mbunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita na Naibu Waziri Mkuu mstaafu, Dkt. Doto Biteko, ameungana na Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Paskasi Muragili, kuwapongeza madiwani pamoja na wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe kwa kuvuka malengo ya ukusanyaji wa mapato ya ndani na kufikia asilimia 109.Dkt. Biteko alitoa pongezi hizo wakati akizungumza na Bukombesasa.blog alisema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya madiwani, wataalamu na viongozi mbalimbali wa Serikali katika kuhakikisha maendeleo ya Wilaya ya Bukombe yanaendelea kupatikana.Alisisitiza umuhimu wa kuendelea kudumisha mshikamano huo ili kuimarisha ukusanyaji wa mapato na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi wa Bukombe.Aidha, Dkt. Biteko alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kupeleka fedha nyingi za miradi ya maendeleo wilayani humo, huku akieleza kuwa viongozi na wataalamu wamekuwa wakisimamia vizuri matumizi ya fedha hizo.Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani wiki iliyopita, Mhandisi Muragili alisema katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026, Halmashauri imeendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali kwa kusimamia ukusanyaji wa mapato kwa ufanisi mkubwa, hali iliyowezesha kufikiwa na kuvukwa kwa malengo yaliyowekwa.“Mafanikio haya yanaonesha kuwa Halmashauri imefikia na hata kuvuka malengo ya ukusanyaji wa mapato, jambo linalotoa matumaini makubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma bora kwa wananchi,” alisema Mhandisi Muragili.Pia aliwapongeza wataalamu na madiwani kwa kazi nzuri wanayoifanya huku akiwasisitiza kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha malengo ya maendeleo yanafikiwa kwa wakati.

Kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo, alisema Serikali itaendelea kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa inakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma stahiki kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Adelina Mfikwa, alisema watumishi wa Halmashauri wataendelea kushirikiana kwa karibu na madiwani katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali, ikiwemo ukusanyaji wa mapato.Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma, alisema madiwani wamejipanga kuendelea kushirikiana na wataalamu ili kuhakikisha maendeleo ya Wilaya ya Bukombe yanaendelea kupatikana kupitia usimamizi mzuri wa mapatona utekelezaji wa miradi ya maendeleo.



Comments