Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita, Evarist Gerevas, amepongezwa na Mbunge wa Jimbo la Bukombe ambaye pia ni Mjumbe wa NEC, Dkt. Doto Biteko, kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuwatumikia wanachama wa chama hicho.
Dkt. Biteko alisema Evarist amekuwa mstari wa mbele kuwashika mkono wanachama katika wilaya mbalimbali anapofanya ziara, kwa kusikiliza na kutatua changamoto zao, ikiwemo suala la upatikanaji wa ofisi za CCM ngazi ya kata.
Pongezi hizo zilitolewa leo Mei 2, 2026, wakati wa ziara ya Dkt. Biteko ya kuwashukuru wanachama wa CCM kwa kumchagua Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, yeye mwenyewe pamoja na madiwani wa Wilaya ya Bukombe.
Akizungumza katika ziara hiyo, Dkt. Biteko alisema Evarist amekuwa akichangia kwa kiasi kikubwa shughuli za chama mkoani Geita kwa kushirikiana na uongozi wa CCM wa mkoa, lengo likiwa ni kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa wanachama.
“Nichukue nafasi hii kumpongeza Evarist kwa kazi nzuri anazozifanya ndani ya chama, hususan kusaidia ujenzi wa ofisi za CCM katika ngazi ya kata kila anapofanya ziara,” alisema Dkt. Biteko.
Katika ziara hiyo, Dkt. Biteko pia alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuwaletea wananchi maendeleo kupitia miradi mbalimbali, ikiwemo sekta za afya, maji, elimu na miundombinu ya barabara.
Aidha, aliwataka wanachama wa CCM kuendelea kudumisha umoja, mshikamano na upendo, pamoja na kuzungumzia mema yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita.
Alihimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika maendeleo yao kwa kuchangia nguvu kazi na rasilimali pale Serikali inapotekeleza miradi ya maendeleo.
“Hakuna nchi inayoweza kuendelea kwa kutegemea Serikali pekee. Wananchi lazima washiriki kikamilifu kwa kujitolea na kushirikiana na Serikali,” alisisitiza.
Akiwa katika Kata ya Bugelenga, Dkt. Biteko alieleza kuwa Serikali ya Rais Samia imeendelea kupeleka fedha za maendeleo katika Wilaya ya Bukombe, ikiwa na lengo la kuibadilisha kiuchumi na kijamii.
Kwa upande wao, madiwani wa kata mbalimbali waliwasilisha mafanikio na changamoto za maeneo yao.
Diwani wa Kata ya Bulenga, Erick Kagoma, alisema Serikali imetoa shilingi milioni 437 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Msingi Kakoyoyo na milioni 337 kwa ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Bulenga. Aidha, milioni 30 zimetolewa kwa ukarabati wa madarasa na milioni 20 kwa ajili ya kukamilisha bweni la wasichana.
Diwani wa Kata ya Ng’anzo, Mashaka Shing’wenda, alimpongeza Dkt. Biteko kwa kusikiliza kero za wananchi na kuchangia maboresho katika sekta ya elimu na afya, ikiwemo ujenzi wa shule ya sekondari.
Naye Diwani wa Kata ya Bugelenga, Donald Lubigisa, alieleza kuridhishwa na maendeleo yanayoletwa kupitia ushirikiano mzuri kati ya Mbunge na Serikali.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Iyogelo, Juma Lushiku, alisema kata yake imepokea zaidi ya shilingi milioni 101 kutoka Serikalini, pamoja na milioni 141 kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati na milioni 100 kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa ajili ya ujenzi wa madarasa.

Comments
Post a Comment