Mbunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Dkt. Doto Biteko, amehitimisha ziara yake ya kutembelea kata zote 17 za jimbo hilo kwa lengo la kuwashukuru wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kumchagua Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, yeye mwenyewe pamoja na madiwani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Akihitimisha ziara hiyo katika kata za Ushirombo, Igulwa na Katente, Dkt. Biteko aliwataka wanachama wa CCM kuendelea kushirikiana, kuimarisha mshikamano na kuelekeza nguvu katika kazi za maendeleo badala ya kujadili masuala ya uchaguzi uliopita.
"Vumilianeni, sameheaneni na msikubali kugawanywa na mtu yeyote. Badala yake tuwe wamoja na tuendelee kusema mazuri yanayofanywa na Rais Dkt. Samia kwa maendeleo ya wananchi wetu," alisema Dkt. Biteko.
Akiwashukuru wanachama wa CCM, Dkt. Biteko alisema nafasi ya ubunge aliyopewa ni dhamana ya wananchi wa Bukombe, na kwamba ataendelea kupambana kuhakikisha miradi ya maendeleo inafika katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.
"Ubunge huu mlionipa ni wenu. Nina deni kubwa kwenu na nitaendelea kupambana kuleta miradi ya maendeleo ili Bukombe ifikie hatua kubwa zaidi ya maendeleo. Tuna kazi mbili muhimu kwa Rais Dkt. Samia; kumuunga mkono na kumuombea ili aendelee kuleta fedha za maendeleo," alisema.
Dkt. Biteko alisema Wilaya ya Bukombe ni miongoni mwa maeneo yanayotarajiwa kukua kwa kasi katika miaka ijayo, hivyo aliwataka wananchi kutouza maeneo yao kiholela bali kuyatunza kwani ni fursa ya maendeleo na uchumi wa baadaye.
Aidha, alimpongeza Rais Dkt. Samia kwa juhudi kubwa za kupeleka fedha za miradi ya maendeleo, akisema Serikali inatarajia kujenga kilomita 15 za barabara za lami na kuhakikisha hata Kata ya Uyovu inanufaika na miundombinu hiyo.
Aliongeza kuwa Bukombe ya baadaye itakuwa na vivutio mbalimbali ikiwemo uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu unaotarajiwa kukamilika hivi karibuni, pamoja na soko na stendi ya kisasa ambazo ujenzi wake unaendelea.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukombe, Luhanda Lutonja, alisema ziara hiyo ilianza Aprili 7, 2026 na kuhitimishwa Mei 23, 2026 kwa lengo la kuwashukuru wanachama wa CCM kwa kumchagua Rais Dkt. Samia, Mbunge pamoja na madiwani.
"Nimpongeze Dkt. Biteko kwa kuona umuhimu wa kurudi kwa wanachama na kutoa neno la shukrani. Hii inaonesha moyo wa upendo na kuthamini mchango wa wanachama wa chama. Sasa zamu ya wananchi wote inakuja kupitia mikutano ya hadhara," alisema Lutonja.
Diwani wa Kata ya Katente, Tabu Ng'hwani, alisema wanachama walikuwa wamemkumbuka Mbunge wao na kwamba kupitia juhudi zake, kata hiyo imepokea zaidi ya shilingi bilioni 32 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo barabara, elimu, afya, maji, soko, stendi.
Naye Diwani wa Kata ya Igulwa, Richard Mabenga, alisema huduma ya maji ambayo hapo awali ilikuwa changamoto kubwa sasa imeboreshwa na wananchi wengi wanapata maji safi na salama.
Mabenga alisema kata hiyo pia imepokea shilingi milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati, huku shule ya msingi Kelezia ikikamilika pamoja na uwepo wa chuo kinachoendelea kutoa huduma za elimu.
Aidha, alisema barabara ya lami imejengwa na shilingi milioni 150 zimetolewa kwa ajili ya ununuzi wa gari la Shule ya Bukombe Vision ambalo tayari linatumika kusafirisha wanafunzi.
Diwani wa Kata ya Ushirombo, Lameki Warangi, alisema kata yake itaendelea kumuunga mkono Mbunge na kuimarisha umoja wa wananchi.
Kwa upande wake, Diwani wa Viti Maalum Ester Mafulu alisema Dkt. Biteko hajawahi kubadilika tangu aingie bungeni na kwamba amebadilisha mazingira ya maendeleo katika maeneo mengi ya Bukombe.
Diwani wa Viti Maalum Leokadia Kasase alisema hatua ya Mbunge kuwashukuru wanachama inaonesha ushirikiano mzuri uliopo kati yake, chama, serikali na wananchi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma, alisema miradi mbalimbali ya maendeleo inaendelea kutekelezwa na mingine tayari imeanza.
Aidha, aliwaomba wazazi na walezi kuendelea kupeleka watoto katika Shule ya Bukombe Vision ambapo kupitia juhudi za Mbunge Dkt. Biteko, Serikali ilitoa zaidi ya shilingi milioni 100 kwa ajili ya ununuzi wa gari jipya la kubeba wanafunzi ambalo tayari linafanya kazi.

Comments
Post a Comment