DKT. BITEKO AHAMASISHA WANANCHI KUJENGA NYUMBA BORA KWA KUZINGATIA MPANGO MIJI


Na,ErnestMagashi

ebukombesasa.blogspot.com.tz

Wananchi wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wametakiwa kujenga nyumba bora kwa kuzingatia sheria na kanuni za mipango miji, ikiwemo kuheshimu mipaka ya barabara ili kuweka mazingira mazuri ya maendeleo ya sasa na ya baadaye.Wito huo umetolewa na Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Dkt. Doto Biteko, wakati wa ziara yake katika Kata ya Bulangwa kwa ajili ya kuwashukuru wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, yeye pamoja na madiwani wakati wa uchaguzi mkuu 2025.Akizungumza na wanachama wa CCM Dkt. Biteko alisema anaiona Bukombe ya miaka ijayo ikiwa katika hatua kubwa ya maendeleo tofauti na ilivyo sasa, hivyo wananchi wanapaswa kutunza ardhi zao na kujenga nyumba bora kwa kuzingatia mipango ya maendeleo ya miji.Alisema kuwa Wilaya ya Bukombe inaendelea kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi kutokana na uwepo wa mgodi wa kati wa madini ya dhahabu, maendeleo ya miundombinu ikiwemo kiwanja cha mpira wa miguu pamoja na fursa nyingine zinazotarajiwa kuibuka katika siku zijazo."Nawaomba wananchi wa Bulangwa na Bukombe kwa ujumla tujenge nyumba bora na kuzingatia mipaka ya barabara. Tusikubali kushawishiwa kuuza maeneo yetu kiholela, badala yake tuyatumie kama fursa za uwekezaji na maendeleo yanayoletwa na Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan," alisema Dkt. Biteko.Aidha, Dkt. Biteko alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuendelea kupeleka fedha za miradi ya maendeleo kwa wananchi wa Bukombe na taifa kwa ujumla. Pia aliwataka wanachama wa CCM kuendelea kueleza wananchi kazi zinazofanywa na serikali katika kuboresha huduma mbalimbali ikiwemo sekta ya afya.Pia aliwasisitiza wanachama kuwa wamoja na kuepuka migawanyiko inayoweza kurudisha nyuma maendeleo ya Wilaya ya Bukombe. Alieleza kuwa anatamani Zahanati ya Bulangwa ipandishwe hadhi na kuwa Kituo cha Afya ili wananchi wapate huduma karibu badala ya kufuata huduma hizo mjini Ushirombo.Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Bulangwa, Yusuph Mohamed, alisema kata hiyo imepokea shilingi milioni 3.8 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya msingi sambamba na utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo.Naye Mwenyekiti wa Halmashauri, Erick Karma, alimpongeza Dkt. Biteko kwa juhudi zake za kushirikiana na serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo, akieleza kuwa halmashauri imepokea zaidi ya shilingi bilioni 11 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Kata ya Bulangwa, Alexzanda Mtuzya, alisema wananchi wanaendelea kuona maendeleo yanayotekelezwa na hivyo wana imani na uongozi wa Mbunge huyo. Alisema Dkt. Biteko anapaswa kutembea kifua mbele kutokana na namna wananchi wanavyomuunga mkono.


Comments